
Mkurugenzi Mtendaji wa MUWASA, Esther Gilyoma, alifanya ziara ya kukagua maendeleo ya utekelezaji wa Mradi wa Maji wa Miji 28 wa Serengeti, Septemba 9, 2026. (Na Mpigapicha Wetu)
Serengeti
-----------------
Utekelezaji wa Mradi wa Maji wa Miji 28 wa Wilaya ya Serengeti mkoani Mara umefikia asilimia 82, Mkurugenzi Mtendaji (MD) wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Musoma (MUWASA), Esther Gilyoma, amesema.
MD Gilyoma aliyasema hayo Septemba 9, 2026, alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya utekelezaji wa mradi huo katika eneo la Bwawa la Manchira kwa gharama ya shilingi zaidi ya bilioni 21 kutoka serikalini.
“Tumetembelea mradi wetu huu wa miji 28 wa Serengeti, kazi ni nzuri, kwa sasa utekelezaji umefikia asilimia 82,” alisema MD Gilyoma mbele ya waandishi wa habari.
Kwa mujibu wa MD huyo wa MUWASA, mradi huo unahusisha ujenzi wa chanzo cha maji, kituo cha kuchuja maji, mtandao wa bomba wenye urefu wa kilomita 31 na tanki la kuhifadhi maji lenye uwezo wa lita 2,000,000.

Mradi huo ambao unatekelezwa na Mkandarasi Mega Engineering and Infrastructure Company Limited na kusimamiwa na Mkandarasi Mshauri WAPCOS LIMITED, unatarajiwa kuboresha na kuimarisha huduma ya majisafi na salama kwa wakazi zaidi ya 160,000.
MD Gilyoma alitoa shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuidhinisha fedha zinazogharimia utekelezaji wa mradi huo.
“Tunamshukuru Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kuwezesha miradi kama hii kutekelezwa katika mkoa wetu wa Mara.
“Miradi hii ni mikubwa na inahitaji rasilimali fedha, kama mnavyoona mradi huu unagharimu shilingi zaidi ya bilioni 21, si haba,” alisema MD Gilyoma.
Hivyo, alimtaka mkandarasi wa mradi huo kuongeza kasi ya utekelezaji ili ukamilike haraka na kuwezesha wananchi wanaolengwa kunufaika na huduma ya maji.

MD Gilyoma alisema MUWASA itaendelea kusimamia utekelezaji wa maelekezo ya serikali kupitia Wizara ya Maji, chini ya uongozi wa Waziri Jumaa Aweso na Katibu Mkuu, Mhandisi Mwajuma Waziri.
“Nishukuru serikali yangu sikivu kupitia Wizara ya Maji ikiongozwa na Mhe. Jumaa Aweso na Katibu Mkuu wetu, Mwajuma Waziri, kwa namna ambayo wametoa maelekezo… sisi tuko hapa kuyatekeleza,” alisema MD Gilyoma.
Aliendelea: “Tutasimamia kazi kama walivyoelekeza. Kazi ziko vizuri na sasa tumemwagiza mkandarasi aharakishe ili angalau tu- inject maji katika bomba ili wananchi waendelee kufurahia huduma ya maji itolewayo na serikali yao.”
Septemba 13, mwaka jana, Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma alifanya ziara ya kukagua maendeleo ya utekelezaji wa mradi huo na kumtaka mkandarasi kuongeza nguvu kazi na vifaa ili ukamilike haraka.

Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri, akiongozwa na mkandarasi alipokwenda kukagua maendeleo ya utekelezaji wa mradi huo, Septemba 13, 2026. (Picha ya Maktaba)
Kukamilika kwa mradi huo kunatarajiwa kutatua changamoto ya maji kwa wakazi wa mji wa Serengeti na maeneo jirani, sambamba na kuchochea shughuli za kijamii na kiuchumi zinazotegemea upatikanaji wa huduma hiyo muhimu.
Diwani wa Viti Maalum katika Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, Salome Mabelele, alisema wananchi wanausubiri mradi huo kwa shauku kubwa wakiamini utakuwa mwarobaini wa uhaba wa maji katika mji huo.
“Tuna matumaini makubwa kwamba mradi huu utawezesha mji wa Serengeti kupata maji ya uhakika na hivyo kutuondolea kero ya uhaba, mgawo na kukatika ovyo kwa maji ya bomba,” alisema Salome.
Naye Diwani wa Kata ya Stendi Kuu, Mwita Joseph maarufu kwa jina la Mapancha, alisema Mradi wa Maji wa Miji 28 wa Serengeti utakuwa mkombozi kwa maelfu ya wakazi wa kata nane, ikiwemo Manchira.
“Mradi huu utatuondolea adha kubwa ya uhaba wa maji kwa sababu utaongeza uzalishaji wa maji ya bomba kutoka lita 300,000 hadi 2,000,000 katika mji wa Serengeti,” alisema Mapancha.
Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Samia, imeendelea kuongeza uwekezaji katika uboreshaji na uimarishaji wa huduma ya maji mijini na vijijini.
No comments:
Post a Comment