NEWS

Tuesday, 27 October 2026

DC Tarime ataka Hifadhi ya Serengeti kuwapa wananchi wa vijiji jirani kipaumbele fursa za ajira, biashara



Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele, akizungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika jana Jumanne katika kijiji cha Kegonga kinachopakana na Hifadhi ya Taifa Serengeti.

Na Christopher Gamaina
Tarime
-----------

Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele, ameitaka Hifadhi ya Taifa Serengeti kuwapa kipaumbele wananchi wa vijiji vinavyopakana nayo katika fursa za ajira na biashara mbalimbali zinazohitajika hifadhini.

Amesema hali hiyo itajenga na kuimarisha uhusiano na ujirani mwema baina ya pande hizo mbili na kuchochea maendeleo ya kijami, kiuchumi na uhifadhi endelevu katika maeneo hayo.

Meja Gowele aliyasema hayo baada ya kusikiliza changamoto za wananchi katika mikutano ya hadhara iliyofanyika kwa nyakati tofauti jana Jumanne katika vijiji vya kata za Gorong’a na Nyanugu zinazopakana na hifadhi hiyo wilayani Tarime.

Sehemu ya wananchi wakifuatilia hotuba ya Mkuu wa Wilaya katika mkutano wa hadhara kijijini Masanga.

“Vijana na wanawake kutoka vijiji hivi wapewe kipaumbele cha kazi, zikiwemo za muda mfupi na biashara zinazohitajika hifadhini, ili waweze kujikwamua kiuchumi,” alisema Meja Gowele.

Alisisitiza kuwa uhifadhi endelevu unapaswa kwenda sambamba na ustawi wa jamii zinazoishi jirani na maeneo yaliyohifadhiwa.

Mkazi wa kata ya Gorong'a akiwasilisha maoni yake kwa Mkuu wa Wilaya katika mkutano wa hadhara.

Meja Gowele alisema hifadhi ina wajibu wa kuwasaidia wananchi hao kutatua changamoto za huduma za kijamii zinazowakabili, hususan upatikanaji wa maji kwa matumizi ya nyumbani na mifugo, uboreshaji wa miradi ya elimu, afya na barabara.

Aidha, aliwataka askari wa hifadhi kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria na miongozo, ikiwemo kuepuka vitendo vya uonevu na unyanyasaji dhidi ya wananchi wanaokamatwa kwa tuhuma za kufanya uhalifu hifadhini.

Mkazi mwingine wa kata ya Gorong'a akiwasilisha kwa Mkuu wa Wilaya changamoto za wananchi katika mkutano wa hadhara kijijini Masanga

Kwa upande mwingine, Meja Gowele aliwataka wananchi hao kujiepusha na vitendo vya ujangili, ikiwemo uwindaji haramu na kuingiza mifugo hifadhini.

Mkuu huyo wilaya alisema uhifadhi unahitaji ushirikiano wa pande zote, hivyo wananchi hao wanapaswa kuheshimu sheria na mipaka ya hifadhi hiyo.

Vilevile, aliwataka wananchi watakaopata ajira katika hifadhi hiyo, zikiwemo za muda mfupi, kuwa waaminifu, waadilifu na kutunza mali za hifadhi na watalii.

“Vijana mnaopata ajira muwe waaminifu ili kujijengea imani kwa hifadhi,” alisema.

Mkazi wa kata ya Nyanungu akimweleza Mkuu wa Wilaya changamoto za wananchi wa kata hiyo katika mkutano wa hadhara kijijini Kegonga

Kuhusu mvutano wa mpaka kati ya hifadhi na vijiji hivyo, Meja Gowele aliwataka kuwa watulivu na wavumilivu wakati wakisubiri maamuzi ya viongozi wa ngazi za juu serikalini.

Aliwahimiza wananchi kuendelea kutumia njia za mazungumzo na kufuata taratibu za kushughulikia suala hilo, huku wakiepuka vitendo vinavyoweza kuongeza mvutano kati yao na mamlaka za uhifadhi.

Afisa Mahusiano ya Jamii wa Hifadhi ya Taifa Serengeti, Mhifadhi Abed Mwesigwa, akijibu hoja za wananchi katika mkutano wa hadhara kijijini Kegonga.

Mkuu wa Wilaya alihitimisha kwa kuitaka Hifadhi ya Serengeti kushirikiana na serikali kuitisha mikutano ya mara kwa mara ili kujadiliana na wananchi hao kuhusu namna nzuri ya kujenga uhusiano na ujirani mwema kwa manufaa ya pande zote mbili.

“Mikutano kama hii ni muhimu katika kutafuta suluhu ya changamoto, kujenga mahusiano na ujirani mwema kati ya wananchi na hifadhi,” alisema Meja Gowele.

Awali, wananchi wa vijiji hivyo walimweleza Mkuu wa Wilaya kwamba wako tayari kujenga na kuimarisha uhusiano na hifadhi hiyo iwapo changamoto zinazowakabili zitapatiwa ufumbuzi wa kudumu.

Mkuu wa Wilaya Meja Gowele (kushoto) akimsikiliza mmoja wa wazee katika mkutano wa hadhara kijijini Kegonga.

“Sisi wananchi tuko tayari kwa mahusiano na ujirani mawema, lakini tunaomba hifadhi itusaidie kuboresha huduma za kijamii, vijana wetu wapewe nafazi za ajira hifadhini na wahifadhi wadhibiti tembo wanaotuvamia vijijini,” alisema Anatory Chacha Range.

Pia, wananchi hao waliomba kujengewa uelewa wa masuala ya uhifadhi na umuhimu wake kwa maendeleo ya jamii na taifa, ombi ambalo wahifadhi waliahidi kulifanyia kazi kwa vitendo.

Mhifadhi akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara kijijini Kegonga, Nyanugu. (Picha zote na Mara Online News)

Mkutano mwingine unafanyika leo Jumatano, ambapo Mkuu wa Wilaya, Meja Gowele atahutubia wananchi katika kata ya Kwihancha inayopakana na hifadhi hiyo.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages