![]() |
| Mkuu wa Mkoa wa Mara, Brigedia Jenerali Evans Mtambi. |
Na Mwandishi Wetu
Mara
-----------
Mara
-----------
Mkuu wa Mkoa wa Mara, Brigedia Jenerali Evans Mtambi, leo Jumatatu, amekabidhi tuzo za usafi wa mazingira za Septemba na Oktoba 2026 kwa halmashauri zilizofanya vizuri na kinyago kwa iliyofanya vibaya katika usimamizi wa usafi huo.
Akizungumza katika utoaji wa tuzo hizo, Brigedia Jenerali Mtambi amesema mkoa wa Mara hautavumilia uchafu wa mazingira ikiwa ni pamoja taka za chupa na karatasi za plastiki ambazo ni hatari kwa afya ya mifugo, wanyamapori na mazalia ya samaki.
"Uchumi wa mkoa wa Mara kwa kiasi kikubwa unategemea sekta za ufugaji, utalii [wa wanyamapori] na uvuvi, uchafu ukikithiri hususan kwa kutupa ovyo taka za plastiki unahatarisha uchumi wa wananchi mmoja mmoja na mkoa kwa ujumla," ameonya
Katika mashindano hayo ya usafi wa mazingira, Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti imeibuka mshindi wa kwanza, ikifuatiwa na Manispaa ya Musoma na Mji wa Tarime ambazo zimepewa tuzo na hati za pongezi.
Kwa upande wake Halmashauri ya Wilaya ya Tarime imeshika nafasi ya mwisho katika mashindano hayo na kukabidhiwa kinyago.
Mkuu wa Mkoa amesema mashindano hayo ni endelevu na kwamba yatafanyika kila mwezi ili kulinda afya na uchumi wa wananchi na mkoa kwa kuhakikisha kuwa suala la usafi wa mazingira linakuwa endelevu.

No comments:
Post a Comment