
Kutoka kulia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Suma JKT, Meja Jenerali (Mstaafu) Michael Isamuhyo, Mbunge wa Jimbo la Musoma Mjini, Mgore Miraji, Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini, Esther Matiko, Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Brigedia Jenerali Evans Mtambi, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Patrick Chandi Marwa na MNEC Christopher Gachuma, katika picha ya pamoja mara baada ya kushiriki kikao maalum cha kujadili maendeleo ya mkoa huo kilichofanyika CMG Hotels Tarime, jana Alhamisi.
Tarime
--------------
Viongozi, wafanyabiashara na wadau wengine mbalimbali wamekutana katika Kikao Maalum cha Kujadili Maendeleo ya Mkoa wa Mara, wakijikita zaidi kubainisha fursa zilizopo na vinavyoweza kutumika kuinua uchumi kupitia uwekezaji na ajira.
Kikao hicho kilifanyika jana Alhamisi katika Hoteli ya CMG mjini Tarime chini ya uratibu wa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mara, Patrick Chandi Marwa, ambapo kilifunguliwa na Mkuu wa mkoa huo, Brigedia Jenerali Evans Mtambi, aliyemwakilisha Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Rhimo Nyansaho, kama mgeni rasmi.

Wajumbe wengi walichambua fursa zilizopo kwenye sekta za kilimo, madini, utalii, uvuvi, biashara na ushirika, pamoja na umuhimu wa kuimarisha matumizi ya rasilimali hizo ili ziwe chachu ya ukuaji wa uchumi na uboreshaji wa maisha ya wana-Mara.
Wachangiaji wakuu walikuwa Brigedia Jenerali Mtambi, mfanyabiashara maarufu na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Christopher Mwita Gachuma, Mkurugenzi wa Kemanyanki Contractors, Nicolaus Mgaya "Chichake", Mbunge wa Jimbo la Tarime Mjini, Esther Matiko na Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini, Mwita Waitara, miongoni mwa wadau wengine.

Mkurugenzi wa Mara Online, Jacob Mugini akitambulisha wajumbe kikaoni
Kuhusu uchechemuzi wa maendeleo, Brigedia Jenerali Mtambi alisema sekta binafsi ina nafasi kubwa katika kuchochea ukuaji wa uchumi kupitia uwekezaji kwenye miradi mbalimbali.
Brigedia Jenerali Mtambi akizungumza katika kikao hicho
“Ninatoa wito hata kwa wana-Mara waliopo nje ya Mara waje kuwekeza huku ili ndugu zao wapate ajira, kuinua uchumi na kuleta maendeleo endelevu katika mkoa huu,” alisema Brigedia Jenerali Mtambi.

Sehemu ya wajumbe wakifuatilia mada kikaoni
MNEC Gachuma akisisitiza jambo katika kikao hicho
“Wazo hili ni jambo jema sana, Mwenyekiti [Chandi] umefanya jambo la maana sana. Maendeleo yanaletwa na wenye eneo wenyewe. Mara itajengwa na wana-Mara wenyewe,” alisema Gachuma.

Sehemu nyingine ya wajumbe wakifuatilia mada kikaoni
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kampuni ya Kitalii ya Nyamoyo Adventure kutoka wilayani Serengeti, Baraka Thobias, alitaja vivutio vikubwa vya utalii vilivyopo Mara vyenye fursa za uwekezaji kuwa ni pamoja na Hifadhi ya Taifa Serengeti, Mto Mara, Ziwa Victoria na Makumbusho ya Mwalimu Julius K. Nyerere - Butiama.

Baraka akiwasilisha mada katika kikao hicho
Mkurugenzi wa Kemanyanki Contractors, Chichake, yeye alitoa wito kwa wafanyabiashara wa ndani kuchangamkia fursa za kusambaza bidhaa na huduma mbalimbali zilizopo katika Mgodi wa Dhahabu wa North Mara.
Chichake akichangia mada katika kikao hicho
Mbunge Waitara yeye alitoa wito kwa wana-Mara yenye nyadhifa za juu kwenye utumishi wa umma kujitokeza kutoa michango ya hali na mali ili kusukuma maendeleo ya kisekta katika mkoa huo.

Mbunge Waitara akichangia mada kikaoni
Kwa upande wake Mbunge Esther Matiko pamoja na mambo mengine, alishauri mkoa uwe na database (hifadhidata) ya vijawa wake na viwango vyao vya elimu na taaluma ili fursa zinapotokea iwe rahisi kujua wanaostahili kupewa.

Mbunge Esther Matiko akizungumza kikaoni
Katika kuhitimisha kikao hicho, Mwenyekiti Chandi na Mkuu wa Mkoa, Brigedia Jenerali Mtambi, waliwahakikishia wajumbe kuwa kikao hicho ni mwanzo wa vikao endelevu vya kujadili maendeleo ya mkoa huo.
Mwenyekiti Chandi akisisitiza uendelevu wa vikao vya aina hiyo mkoani Mara. (Picha zone na Mara Online News)





No comments:
Post a Comment