NEWS

Thursday, 8 October 2026

Kituo cha Wageni chazinduliwa rasmi Hifadhi ya Taifa Serengeti



Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Hamad Hassan Chande (katikati) katika uzinduzi rasmi wa Kituo cha Wageni Serengeti jana Oktoba 7, 2026. Kushoto ni Balozi wa Ujerumani nchini Tanzania, Annett Günther na kulia ni Kamishna wa Uhifadhi wa TANAPA, Massana Mwishawa.

Na Godfrey Marwa
Serengeti
----------------

Kituo cha Wageni Serengeti (Serengeti Visitors Centre) umezinduliwa rasmi katika eneo la Seronera ndani ya Hifadhi ya Taifa Serengeti, chini ya Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA).

Ujenzi na uboreshaji wa kituo hicho umefadhiliwa na Serikali ya Ujerumani kupitia Wizara ya Shirikisho ya Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo (BMZ) na Benki yake ya Maendeleo (KfW).

Hatua hiyo imefikiwa chini ya Mradi wa Maendeleo na Uhifadhi wa Mfumo wa Ikolojia ya Serengeti (SEDCP) na kutekelezwa na TANAPA kwa ushirikiano na Shirika la Uhifadhi la Frankfurt Zoological Society (FZS).

Lengo la kituo hicho ni kutoa taarifa, elimu ya uhifadhi, kukuza uelewa wa umuhimu wa Hifadhi ya Serengeti na utalii endelevu kwa kizazi cha sasa na vijavyo.

Akifungua kituo hicho jana Jumatano, Oktoba 7, 2026, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Hamad Hassan Chande, akiambatanana Balozi wa Ujerumani hapa nchini, Annett Günther, aliishukuru Serikali ya Ujerumani kwa ushirikiano wa vitendo katika utekelezwaji wa miradi ya uhifadhi na utalii.

Naibu Waziri Chande (katikati) akikata utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa kituo hicho. Kulia ni Balozi Annett Günther na kushoto ni Kamishna wa Uhifadhi wa TANAPA, Massana Mwishawa.

Chande alisema kituo hicho kitawezesha wageni wanaotembelea eneo hilo kupata taarifa kuhusu umuhimu wa Hifadhi ya Serengeti kwa manufaa ya Tanzania na dunia.

"Kituo hiki kitaleta ufanisi mkubwa sana kwa wageni wanaokuja kutembelea Hifadhi ya Serengeti, watapata taarifa zenye weledi hapa kabla ya hawajaenda kujionea utajiri wa vivutio tulivyonavyo ndani ya Hifadhi ya Serengeti.

“Tunataka kila mtalii awe anaondoka Hifadhi ya Serengeti akiwa na uelewa mpana wa wanyamapori aliowaona na ikolojia wanayoishi," alisNaibu Waziri Chande alisema katika sehemu ya hotuba yake.

Naibu Waziri Chande akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa kituo hicho

Awali, Kamishna wa Uhifadhi wa TANAPA, Massana Mwishawa, alisema Kituo cha Wageni Serengeti ni mahususi kwa ajili ya taarifa za uhifadhi na shughuli wanazofanya kwa wananchi, wageni, vikundi vya kitaaluma na watafiti mbalimbali wanaotembelea hifadhi hiyo.

"Hili ni tukio lenye maana zaidi ya tatu, kuzindua kituo, kusherekea miaka 65 ya ushirikiano kati ya Tanzania na Ujerumani katika shughuli za uhifadhi Pamoja na kutimiza miaka 75 ya kuanzishwa kwa Hifadhi ya Taifa Serengeti.

"TANAPA tuna furaha kubwa, kituo hiki kinaenda kuongeza chachu ya shughuli tunazofanya kama hifadhi, watalii wanapokuja wanaweza kuijua Tanzania kupitia kituo hiki pamoja na taarifa zote kuhusu Serengeti na uhifadhi,” alisema Kamishna Mwishawa.

Aliongeza kuwa kupitia kituo hicho, wanaenda kuongeza taarifa zinazohusiana na jamii, akisisitiza kuwa bila jamii hakuna uhifadhi.

"Mwanzo tulikuwa na taarifa za uhifadhi na utalii zaidi lakini sasa tunaenda kuongeza taarifa zinazohusiana na jamii, maana bila jamii hifadhi itatetereka,” alisema Kamishna Mwishawa na kuongeza:

“Tunaenda kuonesha kumbukumbu za kuwepo kwa binadamu aliyekuwa anaishi na wanyamapori miaka hiyo kabla Serengeti haijawa Hifadhi ya Taifa, kuhakikisha uhifadhi na utalii unakuwa endelevu.”

Kikundi cha ngoma ya asili kikitumbuiza katika hafla ya uzinduzi wa kituo hicho. (Picha zote na Mpigapicha Wetu)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages