NEWS

Sunday, 11 October 2026

Mtanzania Jihan Dimack atwaa Taji la Miss Grand International 2026



Jihan Mohin Dimack akifurahia kutwaa ushindi wa Taji la Miss Grand International 2026

BANGKOK, Thailand

Mtanzania Jihan Mohin Dimack ameandika historia baada ya kutwaa Taji la Miss Grand International 2026 katika fainali zilizofanyika usiku wa Oktoba 10, 2026, jijini Bangkok, Thailand.

Ushindi huo unamfanya Jihan kuwa mwanamke wa kwanza kutoka Afrika kushinda mashindano hayo ya urembo ya kimataifa tangu yalipoanzishwa mwaka 2013.

Jihan aliyeiwakilisha Tanzania katika mashindano hayo, aliwashinda washiriki wengine 79 kutoka mataifa mbalimbali na kutangazwa mshindi wa jumla, huku nafasi ya pili ikichukuliwa na Shyare Andrade wa Ecuador.

Safari ya Jihan katika mashindano ya urembo ilianza miaka kadhaa iliyopita, ambapo mwaka 2014 alishika nafasi ya tatu katika mashindano ya Miss Tanzania.

Mwaka 2016 alitwaa Taji la Miss Universe Tanzania na mwaka huu (2026) alirejea tena katika mashindano ya urembo na kutwaa Taji la Miss Grand Tanzania lililomwezesha kushiriki mashindano ya kimataifa.

Ushindi huo wa Jihan unaongeza sifa kwa Tanzania katika jukwaa la urembo duniani, hasa wakati huu ambapo taifa linatarajiwa kuwa mwenyeji wa mashindano ya Miss World yatakayofanyika mwakani (2027).

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages