NEWS

Sunday, 11 October 2026

Vijana Musoma Vijijini wanufaika na mikopo ya shilingi bilioni 1.26



Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini, Prof. Sospeter Muhongo.

Na Mwandishi Wetu
Musoma
-----------------

Vijana 194 katika Jimbo la Uchaguzi la Musoma Vijijini mkoani Mara wamepata mikopo ya shilingi bilioni 1.26 kwa ajili ya kuendesha shughuli za uvuvi na ufugaji ili kuinua kipato chao.

Kijiografia, jimbo la Musoma Vijijini lina kata 21, kati ya hizo, 18 zimepakana na Ziwa Victoria na kuwa na fursa kikubwa ya shughuli za uvuvi.

Taarifa iliyotolewa hivi karibuni na Ofisi ya Mbunge wa jimbo hilo, Prof. Sospeter Muhongo, ilieleza kuwa vijana 194 waliopata mikopo ni kati ya 421 waliotuma maombi ya kwanza ya mikopo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi na Benki ya Kilimo Tanznaia (TADB).

Taarifa hiyo ilifafanua kuwa vijana waliofanikiwa kupata mikopo wamejikita katika uvuvi na ufugaji ambazo ndizo shughuli kuu katika jimbo hilo ukiachilia mbali kilimo na biashara mbambali.

Pia, taarifa hiyo ilieleza kwamba katika awamu ya pili, vijana 750 wametuma maombi ya kupata mikopo isiyokuwa na riba ili kukuza uchumi wao.

Kupatikana kwa mikopo kwa vijana ni jitihada za makusudi zinazofanywa na Mbunge Prof. Muhongo ili kupambana na umaskini katika jimbo la Musoma Vijijini lenye vijiji 68.

Mbunge huyo alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuwezesha kupatikana kwa mitaji na ajira kwa vijana ili waweze kujitegemea kiuchumi.

Pia, aliishukuru Wizara ya Mifugo na Uvuvi na Benki ya TADB kwa kutoa mikopo ya kuimarisha shughuli za ujasiriamali kwa vijana.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages