
Nyangwine (aliyevaa kofia) akijadiliana na wawekezaji wa nchini Uturuki wakati wa ziara yake jijini Konya hivi karibuni.
Na Mwandishi Wetu
Kongamano Kimataifa la Biashara na Uwekezaji litakalowavuta wadau kutoka mataifa mbalimbali litafanyika jijini Dar es Salaam, Tanzania siku ya Jumapili, Oktoba 11, 2026, kwa mujibu wa waandaaji wa kongamano hilo, Nyambari Nyangwine Group of Companies Limited (NNGCL).
Mgeni rasmi katika kongamano hilo anatarajiwa kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Deogratius Ndejembi.
Kongomano hilo litafanyika sambamba na uzinduzi wa vitabu vitatu ambavyo vinatangaza vivutio vya utalii kitaifa na kimataifa.
Vitabu hivyo vimeandikwa na Benson Nyambari Nyangwine, ambaye ni mtoto wa Mwenyekiti wa kampuni hiyo ya NNGCL, Nyambari Nyangwine.
“Hili litakuwa kongamano la kwanza na tutakuwa tunafanya makongamano kama haya Oktoba 11-12 kila mwaka,” amesema Nyambari pia ni mwandishi na mchapishaji maarufu wa vitabu nchini Tanzania.
Taarifa ya NNGCL inafafanua kuwa kongamano hilo litawakutanisha wafanyabiashara, wawekezaji, wajasiriamali, viongozi wa taasisi na wadau mbalimbali wa maendeleo kutoka ndani na nje ya bara la Afrika.
Lengo kubwa la kongamano hilo, kwa mujibu wa NNGCL, ni kukuza ushurikiano wa kibiashara, uwekezaji, kujenga ushirikiano wa kimkakati, kubadilishana uzoefu, maarifa na kufungua fursa mpya za biashara na uwekezaji hapa nchini.
Nyambari Nyangwine na mtoto wake, Benson, wakiwa ziarani nchini Brazil hivi karibuni.
Tayari wageni kutoka nchi mbalimbali wamethibitisha kushiriki katika kongamano hilo la biashara na uwekezaji linalotarajiwa kuwa kivutio kikubwa jijini Dar es Salaam.
Nchi hizo ni pamoja na Poland, Uturuki, Dubai, China, India, Israel, Burundi, Kenya, Uganda, Zambia, Congo, Indonesia, Qatar na Saudi Arabia ambazo Nyambari Nyangwine anafanya nazo biashara.
Mbali na biashara, Nyambari pia ni mwanasiasa ambaye amewahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Tarime mkoani Mara kupitia chama tawala - CCM.
Washiriki wa kongamano hilo wanawakilisha sekta za uchumi na uwekezaji kama vile usafiri na usafirishaji, utalii, uchapishaji, elimu, kilimo, afya, madini, viwanda, nishati, ujenzi wa majengo na miundombinu, miongoni mwa maeneo mengine.
"Tunatarajia kongamano hili litakuwa fursa adhimu kwa wafanyabiashara na wajasiriamali wa Tanzania kukutana na wenzao kutoka mataifa mbalimbali," imeeleza taarifa hiyo na kuongeza: "Mikutano hiyo inalenga kuwezesha uanzishwaji wa ubia wa kimkakati, upatikanaji wa mitaji, teknolojia, utaalamu na nasoko mapya."
Katika kongamano hilo, wafanyabiashara wa Tanzania watapata nafasi ya kutangaza na kutambulisha bidhaa na huduma zao mbalimbali katika medani ya kimataifa, taarifa hiyo imefafanua.
Aidha, kongamano hilo linakusudia kuiweka Tanzania katika ramani ya dunia kama kitovu cha biashara na uwekezaji barani Afrika, kwa kuonesha fursa mbalimbali zinazopatikana katika taifa hili kubwa la Afrika Mashariki.
"Katika kuhakikisha malengo ya kingamano hili yanafikiwa kwa ufanisi, kampuni yetu imeshirikisha Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalumu ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA) ili kushiriki katika kuwafikia wafanyabiashara na wawekezaji wa Kitanzania," ilieleza sehemu ya taarifa ya NNGCL.

No comments:
Post a Comment