NEWS

Monday, 12 October 2026

Serikali yazindua vitabu vya kutangaza vivutio vya utalii vya Tanzania kimataifa vilivyoandikwa na Benson Nyambari Nyangwine




Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
--------------------

Serikali imeipongeza Nyambari Nyangwine Group of Companies Limited (NNGCL) kwa juhudi inazofanya kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo Tanzania kwa kutumia machapisho yanayolenga kufikia hadhira pana zaidi duniani.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Leonard Akwilapo, alitoa pongezi hizo jijini Dar es Salaam, Oktoba 11, 2026 wakati akifungua Kongamano la Kimataifa la Biashara na Uwekezaji lililoambatana na uzinduzi wa vitabu hivyo ambavyo vimeandikwa na Benson Nyambari Nyangwine.

Waziri Akwilapo ambaye alikuwa mgeni rasmi katika kongamano hilo kwa niaba ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Deogratius Ndejembi, alisema matumizi ya lugha mbalimbali katika kutangaza utalii vya utalii yatasaidia kuitangaza Tanzania kimataifa na kuimarisha fursa za uwekezaji katika sekta hiyo.

Alisema utalii ni miongoni mwa sekta zenye uwezo wa kuchangia mapato ya taifa, kutengeneza ajira na kukuza biashara za usafiri, malazi, vyakula, sanaa na utamaduni.

Mtoto Benson Nyambari Nyangwine (aliyevaa koti jeusi) akishirikiana na wengine kukata keki katika kongamano hilo

Aidha, Waziri Akwilapo alimpongeza mfanyabiashara Nyambari Nyangwine ambaye ni Mwenyekiti wa NNGCL, kwa kupanua wigo wa shughuli zake nje ya mipaka ya Tanzania, zikiwemo nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Maziwa Makuu, Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na mataifa mengine.

“Ndugu Mwenyekiti, nakushukuru na nakupa pongezi za dhati kwa kuwa mfano wa kampuni ya Kitanzania inayovuka mipaka na kufanya biashara katika nchi za Afika Mashariki, Maziwa Makuu na SADC,” alisema Waziri Akwilapo.

Waziri Akwilapo alisema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, inathamini sekta binafsi kama mbia halisi wa maendeleo nchini, ikiamini kuwa hakuna taifa linaloendelea bila sekta binafsi imara.

Alisema sekta binafsi inatarajiwa kuchangia takriban asilimia 70 ya uwekezaji unaohitajika kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

“Katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, sekta binafsi inatarajiwa kuchangia takribani asilimia 70 ya uwekezaji wote unaohitajika, huku serikali ikichangia asilimia 30 kupitia rasilimali za umma,” alisema.

Sehemu ya washiriki wakifuatilia jambo katika kongamano hilo

Kwa mujibu wa Waziri Akwilapo, juhudi za kampuni za Kitanzania kuingia katika masoko ya kimataifa ni mfano kwa vijana na wafanyabiashara wengine wanaotaka kukuza biashara zao huku wakichangia maendeleo ya taifa.

Aliwashukuru waandaaji, hususan NNGCL chini ya Mwenyekiti wake, Nyambari Nyangwine, kwa kuandaa kongamano hilo la kimataifa lililowakutanisha wadau mbalimbali kutoka mataifa tofauti duniani.

Alisema uwepo wa wafanyabiashara wa ndani na wa kimataifa, taasisi za umma, wadau wa elimu, utamaduni na utalii unatoa fursa ya kujadili masuala ya maendeleo, kuimarisha uhusiano wa kibiashara, kubadilishana uzoefu, kuanzisha ushirikiano, kubainisha maeneo mapya ya uwekezaji na kuweka mikakati ya kutumia rasilimali zilizopo kwa maendeleo ya taifa.

Hivyo, Waziri Akwilapo alisisitiza kuwa serikali itaendelea kushirikiana na sekta binafsi katika kujenga uchumi wenye ushindani, unaozalisha ajira na kutoa nafasi kwa Watanzania kunufaika na uwekezaji.

Alitumia nafasi hiyo pia kuwakaribisha wawekezaji wa ndani na nje kutumia fursa zilizopo katika sekta mbalimbali nchini kwa uwekezaji wenye faida na kuchangia maendeleo endelevu ya taifa.

Waziri Akwilapo alitoa wito kwa wawekezaji kutumia fursa zilizopo nchini katika kilimo na uongezaji thamani mazao, utalii, viwanda, nishati, uchumi wa buluu na uchumi wa kidijitali.

Alisema serikali itaendelea kuwekeza katika miundombinu ya kisasa, ikiwemo reli, bandari, barabara na mifumo ya nishati ya uhakika, kwa lengo la kupunguza gharama za uzalishaji na biashara, kurahisisha usafirishaji wa bidhaa na kuongeza tija kwa wawekezaji.

Alisisitiza kuwa maendeleo ya miundombinu ni sehemu muhimu ya mkakati wa kuimarisha ushindani wa Tanzania katika kuvutia mitaji kutoka nje, kupanua biashara na kuimarisha nafasi yake kama kitovu cha shughuli za kiuchumi katika Afrika Mashariki na Kati.

Waziri Akwilapo alisema Tanzania ina nafasi ya kimkakati katika biashara ya kikanda kutokana na bandari zake zinazohudumia nchi jirani zisizo na bandari, zikiwemo Uganda, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Zambia na Malawi.

“Aidha, uanachama wa Tanzania katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Eneo Huru la Biashara la Bara la Afrika (AfCFTA) unatoa fursa kwa wawekezaji kufikia masoko mapana zaidi,” aliongeza.

Akizungumzia mwenendo wa uwekezaji, Dkt. Akwilapo alisema, Tanzania imeendelea kuvutia mitaji kutoka nje, akitaja kuwa mwaka 2025 uwekezaji wa moja kwa moja kutoka nje ya nchi (FDI) ulifikia thamani ya dola za Marekani bilioni 1.7.

Aidha, Waziri Akwilapo alisema uwekezaji uliosajiliwa ulifikia dola za Marekani bilioni 10.95 kupitia miradi 915 iliyosajiliwa na Mamlaka ya Uwekezaji Tanzania na Maeneo Maalumu ya Kiuchumi (TISEZA).

Alisema uchumi wa Tanzania unatarajiwa kukua kwa asilimia 6.3 mwaka 2026, huku serikali ikiwa na lengo la kuvutia uwekezaji wa moja kwa moja kutoka nje wenye thamani ya dola za Marekani bilioni 15.

Alisema kufikiwa kwa malengo hayo kunahitaji kuendelea kuboresha mazingira ya biashara, kuimarisha imani ya wawekezaji na kuhakikisha kuwa miradi inayotekelezwa inachangia ukuaji wa uchumi na kuboresha maisha ya wananchi.

Hivyo, Waziri Akwilapo alisema serikali imeendelea kuchukua hatua za kurahisisha taratibu za uwekezaji ili kupunguza ukiritimba na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wafanyabiashara.

Alisema kupitia TISEZA, huduma za mahali pamoja (One Stop Centre) zimewekwa ili kuwawezesha wawekezaji kupata huduma mbalimbali muhimu katika eneo moja, zikiwemo usajili wa kampuni, vibali vya kazi na huduma zinazohusiana na upatikanaji wa ardhi.

Aliongeza kuwa serikali inaendelea kuboresha mifumo ya kodi ili kuifanya iwe rahisi kueleweka na kutekelezeka, pamoja na kuwezesha wawekezaji kupanga shughuli zao za kibiashara kwa muda mrefu.

Kuhusu usalama wa mitaji, waziri huyo alisema Tanzania ni mwanachama wa Wakala wa Kimataifa wa Dhamana za Uwekezaji (MIGA) na Kituo cha Kimataifa cha Utatuzi wa Migogoro ya Uwekezaji (ICSID), taasisi zinazohusika na mifumo ya kimataifa ya ulinzi wa uwekezaji na utatuzi wa migogoro.

Alisema serikali inalenga kuhakikisha kuwa uwekezaji unaoingia nchini unaleta manufaa kwa pande zote, kwa kuhimiza ushirikiano kati ya kampuni za kigeni na za Kitanzania.

Alisema ubia huo unapaswa kuwezesha uhamishaji wa teknolojia, maarifa na ujuzi kwa wataalamu wa ndani, sambamba na kuongeza nafasi za ajira na kuimarisha uwezo wa kampuni za Kitanzania kushindana katika masoko ya kimataifa.

Pia, Waziri Akwilapo alisisitiza kuwa maendeleo ya teknolojia, matumizi ya TEHAMA na Akili Unde (AI) yanaendelea kubadilisha namna shughuli za kiuchumi zinavyofanyika, hivyo Tanzania inapaswa kuendana na mabadiliko hayo ili isiachwe nyuma katika mapinduzi ya nne ya viwanda.

Hivyo, aliwahimiza wafanyabiashara kuwekeza katika mifumo ya kisasa, ubunifu na teknolojia zitakazoongeza ufanisi wa uzalishaji, kupunguza upotevu wa rasilimali na kuboresha utoaji wa huduma.

Alisema matumizi sahihi ya teknolojia yanaweza kusaidia kampuni kuongeza tija, kupunguza gharama za uendeshaji na kufikia wateja wengi zaidi ndani na nje ya nchi.

Aidha, Waziri Akwilapo alisema ushirikiano kati ya serikali, sekta binafsi na taasisi za elimu ni muhimu katika kuandaa rasilimali watu wenye ujuzi unaohitajika katika uchumi unaozidi kutegemea maarifa na teknolojia.

Wageni waliohudhuria kongamano hilo ni kutoka Poland, Uturuki, Dubai, China, India, Israel, Burundi, Kenya, Uganda, Zambia, Congo, Indonesia, Qatar na Saudi Arabia, miongoni mwa nchi nyingine ambazo Nyambari Nyangwine anafanya nazo biashara.

Washiriki hao wanawakilisha sekta za uchumi na uwekezaji kama vile usafiri na usafirishaji, utalii, uchapishaji, elimu, kilimo, afya, madini, viwanda, nishati, ujenzi wa majengo na miundombinu, miongoni mwa maeneo mengine.

Katika kongamano hilo, wafanyabiashara wa Tanzania walipata fursa ya kutangaza na kutambulisha bidhaa na huduma zao mbalimbali katika medani ya kimataifa.

Mtoto Benso akimlisha keki baba yake, Nyambari Nyangwine, katika kongamano hilo.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa NNGCL, Nyambari Nyangwine, kongamano hilo ni fursa adhimu kwa wafanyabiashara na wajasiriamali wa Tanzania kukutana na wenzao kutoka mataifa mbalimbali.

Alisema limelenga kuwezesha uanzishwaji wa ubia wa kimkakati, upatikanaji wa mitaji, teknolojia, utaalamu, masoko mapya na kuiweka Tanzania katika ramani ya dunia kama kitovu cha biashara na uwekezaji barani Afrika, kwa kuonesha fursa mbalimbali zilizopo.

Mbali na biashara, Nyambari Nyangwine pia ni mwanasiasa ambaye amewahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Tarime mkoani Mara kupitia chama tawala - CCM.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages