
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, akiwa na mgeni wake, Rais wa Jamhuri ya Angola, João Manuel Gonçalves Lourenço, ambaye yupo nchini kwa ziara ya kikazi.
Dar es Salaam
-------------------
Tanzania na Angola, nchi ambazo zilikuwa kwenye kundi la nchi sita zilizokuwa mstari wa mbele kupambana na ukoloni na ubaguzi kusini mwa Afrika, sasa zimeungana tena katika vita ya ukombozi wa kiuchumi kwa kuunda ushirikiano wa karibu.
Marais wa nchi hizi, Dkt. Samia Suluhu Hassan wa Tanzania na João Manuel Gonçalves Lourenço wa Angola, wamekubaliana kupanua wigo wa ushirikiano katika sekta muhimu za kiuchumi kama vile mishati, kilimo, miundombinu na ulinzi.
Ushirikiano huu wa nchi hizo, msingi wake uliwekwa na waasasi wa mataifa hayo, Mwalimu Julius Nyerere wa Tanzania na Agostinho Neto wa Angola, wakati wakipambana kuung’oa ukoloni wa Wareno kwenye miaka ya 1960 na 1970.
Rais Lourenco wa Angola aliwasili Tanzania jana Alhamisi, Oktoba 29, 2026, kwa ziara ya siku tatu, ikiwa imepita miaka 45 tangu Rais wa nchi hiyo atembelee taifa hili la Afrika Mashariki.
Katika kuimarisha ushirikiano baina ya nchi hizo mbili kufuatia mazungumzo yaliyofanyika Ikulu ya Dar es Salaam jana, Rais Samia alisema Tanzania itafungua ubalozi wake mjini Luanda, Angola, kuandaa kongamano la biashara na uwekezaji, kuunganisha ushoroba wa Lobito na Dar es Salaam na kuboresha muunganiko wa usafiri wa anga na majini kwa nchi hizo.
Maeneo mengine muhimu yatakayoimarishwa ni sekta za madini na mafuta ili kuzidi kuchochea maendeleo ya kiuchumi kwa mataifa hayo mawili.
Nchi zilizokuwa mstari wa mbele wa ukombozi barani Afrika - Angola, Botswana, Msumbiji, Tanzania, Zambia na Zimbabwe, zinaheshimika barani Afrika kwa kusimama kidete katika kuondoa ukoloni wa Wareno na ubaguzi wa Makaburu huko Afrika Kusini.
Sasa hivi, nchi hizo zimegeukia ushirikiano wa kuleta mabadiliko makubwa ya kiuchumi chini ya Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika Afrika (SADC) yenye wanachama 16.
Ziara ya Rais Lourenco nchini Tanzania inasimama kama kichocheo cha ushirikiano wa muda mrefu wa kindugu baina ya nchi hizo mbili, kwa kufungua milango ya ushirikiano wa kiuchumi, ili kwenda na kasi ya dunia ya mabadiliko yanayotokea katika nyanja mbalimbali za maendeleo.
No comments:
Post a Comment