NEWS

Tuesday, 13 October 2026

Tarime Vijijini: Mgodi wa Barrick wakabidhi miradi mingine mipya ya maendeleo ya jamii serikalini



Viongozi wa Serikali na Idara ya Mahusiano ya Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara wakati wa makabidhiano ya nyumba ya mtumishi wa Zahanati ya Kangariani katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime (Vijijini), Oktoba 12, 2026.

Na Mwandishi Wetu
Tarime
-------------

Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara umekabidhi miradi mingine mipya mitano ya maendeleo ya jamii kwa serikali katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime (Vijijini).

Makabidhiano hayo yalifanyika Oktoba 12, 2026 kwa nyakati tofauti katika kata za Binagi, Nyamwaga, Itiryo, Matongo na Nyarokoba.

Miradi hiyo ni jengo la kufulia na njia za kupita wagonjwa katika Kituo cha Afya Magoma, katani Binagi na barabara ya changarawe yenye urefu wa kilomita 0.75 katani Nyamwaga.

Mingine ni nyumba ya mtumishi wa Zahanati ya Kangariani, katani Itiryo, nyumba ya mtumishi katika Shule ya Sekondari Msege, katani Nyarokoba na barabara ya kuelekea eneo la mashamba katani Matongo.

Miradi hiyo ni miongoni mwa mingine mipya mingi iliyotekelezwa kutokana na fedha zilizotolewa na Mgodi wa Barrick North Mara kupitia mpango wake wa Uwajibikaji kwa Jamii (CSR).

Jengo la kufulia katika Kituo cha Afya Magoma

Akipokea na kukabidhi miradi hiyo kwa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Mkuu wa Wilaya, Meja Edward Gowele, aliushukuru mgodi huo kwa kuendelea kutenga fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya wananchi kupitia mpango wake wa CSR.

Aidha, Meja Gowele aliwataka wakandarasi kuhakikisha miradi ya CSR inayotekelezwa katika halmashauri hiyo inakamilika kwa wakati na kuakisi thamani ya fedha zilizotumika.

"Miradi yote tuitekeleze kama mikataba inavyosema, wananchi wanahitaji kuona matokeo chanya,” alisisitiza

Mkuu huyo wilaya, pia alitoa wito kwa wananchi wa maeneo hayo kushiriki katika ulinzi na utunzaji wa miradi hiyo ili idumu muda mrefu kwa manufaa ya jamii nzima.

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Matera Newland Chacha, aliushukuru mgodi huo akisema utekelezaji wa miradi hiyo itachangia kuboresha huduma za jamii na kuchochea maendeleo kwa wananchi.

Makabidhiano ya nyumba ya mtumishi wa Shule ya Sekondari Msege

“Nyumba hii ya walimu ni kilelezo kuwa miradi hii ya CSR ni mizuri sana. Pia, barabara ni uchumi, maendeleo, na imejengwa kwa wakati hapa Matongo,” alisema Mwenyekiti wa Halmashauri, Chacha.

Kwa upande wao viongozi wa vijiji husika, wakiwemo Emmanuel Wankaba (Nyamwaga) na Matiko Mwita (Kangariani), walisema wamepokea miradi hiyo kwa furaha, huku wakiahidi kuhamasisha wananchi kuilinda kwa ajili ya vizazi vya sasa na vijavyo.

“Wananchi wetu walisharidhia na kupokea hii miradi kwa mikono miwili, mtaalamu wetu ataishi hapa badala ya kwenda kupanga mitaani,” alisema Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Kangariani, Matiko Mwita.

Viongozi wengine walioshiriki katika makabidhiano ya miradi hiyo ni Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Juster Magabe na Meneja Mahusiano wa Mgodi wa Barrick North Mara, Francis Uhadi.

Mradi wa barabara uliotekelezwa katani Nyamwaga. (Picha zote na Mara Online News)

Taarifa zilizopo zinaonesha kuwa tangu mwaka 2019 mgodi huo ulipokabidhiwa kwa kampuni ya Barrick umewekeza shilingi zaidi ya bilioni 31 na kufanikisha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo zaidi ya 250 katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime.

Miradi inayopewa kipaumbele kupitia mpango wa CSR kutoka Barrick North Mara ni ya sekta za elimu, afya, maji, miundombiunu ya barabara, mazingira na uwezeshaji wananchi kiuchumi, hasa vijana.

Mgodi huo unaendeshwa na kampuni ya kimataifa ya uchimbaji madini, Barrick Minig Corporation, kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia kampuni ya Twiga Minerals.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages