
Picha ya pamoja baada ya TARURA Mkoa wa Mara kutoa vifaa vya usafi na utunzaji wa barabara, kisha Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele, kuvikabidhi kwa vikundi 34, leo Oktoba 15, 2026.
Tarime
-------------
Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Mkoa wa Mara imekabidhi vifaa mbalimbali kwa vikundi 34 kwa ajili ya mradi wa usafi na utunzaji wa barabara za Malmshauri ya Mji na Wilaya ya Tarime (Vijijini).
Vifaa hivyo ni pamoja na majembe, koleo, torori, vizibao, gloves, kofia ngumu na viatu vigumu.

Sehemu ya vifaa vilivyokabidhiwa kwa vikundi hivyo
Akizungumza katika hafla ya kukabidhi vifaa na mikataba iliyofanyika mjini Tarime leo Oktoba 15, 2026, Mkuu wa wilaya hiyo, Meja Edward Gowele, amevitaka vikundi hivyo kutekeleza shughuli hizo kwa bidii na uaminifu.
"Fedha zilikuwa zinaenda kwa mtu mmoja (mkandarasi), Rais amesema ziende kwa wananchi, ni neema kwetu, zaidi ya ajira 340 sio kidogo,” amesema Meja Gowele na kuendelea.
"Tunahitaji utu kwenye hii kazi, vifaa mtakavyopewa vikatumike ku- maintain (kuimarisha) barabara, vitunzwe, vilindwe, visiende kufanya kazi nyingine tofauti na barabara.”

Mkuu wa Wilaya, Meja Gowele, akikabidhi vifaa hivyo kwa vikundi hivyo.
Awali, Meneja wa TARURA Mkoa wa Mara, Mhandisi George Tarimo, ameishukuru serikali kwa kutoa kipaumbele kwa makundi maalum ya wananchi.
Aidha, Mhandisi Tarimo ametumia nafasi hiyo pia kuwakumbusha wananchi umuhimu wa kutunza miundombinu ya barabara kwa huduma endelevu.
"Tunamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa mradi huu. Hii ni sehemu ya kusaidia vikundi kukuza vipato vyao kwa kunufaika na asilimia 30 ya bajeti ya manunuzi ya serikali na taasisi za umma,” amesema.
Ameongeza: "Wananchi wa Tarime mjini na vijijini hii fursa, ajira 340. Kwa Tarime hapa tuna shilingi milioni 650, ni matarajio yetu kuwa barabara zetu zitakuwa katika hali nzuri na miji yetu kuwa misafi.”

Mkuu wa Wilaya, Meja Gowele, akikabidhi mikataba ya mradi huo kwa vikundi hivyo.
Nao viongozi na wanachama wa vikundi hivyo wamesema wamepokea mradi huo kwa furaha, huku wakiahidi kufanya kazi kwa bidii ili kujiongezea kipato na kuboresha maisha yao.
"Kazi hii itatusaidia kwa kipato, tunaishukuru serikali kutuona wanakikundi tofauti na mwanzo, tumeomekana watu wa maana, wananchi wategemee kuona barabara zikiwa safi,” amesema Sarah Ryoba Magubo kutoka kata ya Nyerero, Halmashauri ya Wilaya ya Tarime.
Naye Magreth Elia Luhende kutoka kata ya Sabasaba, Halmashauri ya Mji wa Tarime, amesema: "Tumefurahishwa na ujio wa huu mradi, ni ajira itakayokwenda kutuinua kiuchumi, tutafanya usafi kwa weledi.”

Sehemu ya wanachama wa vikundi hivyo wakifurahia kupata mradi huo. (Picha zote na Mara Online News)
No comments:
Post a Comment