
Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere enzi za uhai wake
Miongo zaidi ya sita iliyopita, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, alitamka maneno yatakayoendelea kuishi kwa miaka mingi ijayo kuhusu umuhimu wa sekta ya uhifadhi nchini kama urithi mkubwa ambao Mwenyezi Mungu aliwapa Watanzania.
Jana Oktoba 14, 2026, wakati wa kumbukizi ya miaka 27 ya kifo chake, Watanzania wa tabaka zote katika jamii, walimkumbuka Mwalimu kwa uzalendo na upendo wake kwa nchi yake.
Baba huyu aliibeba Tanzania katika mabega yake mbele ya macho ya jumuiya ya kimataifa na kutaka utajiri wa rasilimali zake utunzwe “kwa niaba ya mababu, kizazi cha leo na vizazi vingine vijavyo.”
Ndiyo maana Septemba 1961, miezi michache kuelekea uhuru wa Tanganyika uliopatikana Desemba 9, Mwalimu Nyerere alitia saini Ilani ya kuwalinda wanyamapori wasiangamizwe ili kuendelea kuwa urithi wa kudumu kwa Watanganyika (Watanzania).
Kwa faida ya Watanzania wa kizazi hiki na vizazi vingine vijavyo, Ilani hiyo ilitamka wazi kwamba: “Kuishi kwa wanyamapori wetu ni suala muhimu kwa sisi wote katika Bara la Afrika. Viumbe hawa wa porini na maeneo wanamoishi siyo tu kwamba ni muhimu kama chanzo cha mshangao na ushawishi, bali ni sehemu ya rasilimali yetu, hatima na ustawi wetu.”
Katika kuwalinda wanyamapori waliowatawanyika katika hifadhi mbalimbali za Tanzania, Mwalimu Nyerere alieleza waziwazi kwamba “hakuna nchi nyingine duniani inayoweza kujisifu kwa kuwa na wanyamapori wengi kama Tanzania.”
“Kwenye Hifadhi ya Serengeti, kuna makundi ya nyumbu. Pale Ziwa Manyara kuna tembo wakila majani kwa amani, faru wanaoga vumbi na kiboko jike na mtoto wake wanacheza ndani ya maji, na kwenye Hifadhi ya Ngorongoro simba wanatafuna kuru waliyemwuua.
“Juu ya mti unasikia nyani wakipiga makelele, na kwa mbali unaweza kusikia sauti ya chui mwenye njaa akiwa mawindoni,” alisema Mwalimu miaka zaidi ya 60 iliyopita, akitilia mkazo namna ya kuhifadhi urithi wa wanyamapori.
Kwanini Baba wa Taifa alitaka uwepo ulinzi madhubuti wa wanyamapori na mazingira wanamoishi? Zipo sababu kadhaa ambazo leo matunda yake tunayaona kama taifa kufuatia maono ya Mwalimu Nyerere.
Tayari, kwa Tanzania ya leo tunachekelea mafuriko ya watalii wanaokuja kutembelea vivutio mbalimbali na kutuletea marundo kwa marundo ya fedha za kigeni ambazo ni muhimu kwa kukuza uchumi wetu.
Kumekuwepo na ongezeko la wanyamapori kwa ajili ya uwindaji, ngozi na bidhaa nyingine. Nchi yetu imejijengea jina maarufu duniani kuwa kituo cha utalii, na kuwepo kwa wanyamapori wengi nchini Tanzania kumewapa nafasi wanasayansi kuja kufanya tafiti mbalimbali za tabia zao.
Hata hivyo, Mwalimu Nyerere alionya kwamba hifadhi za taifa na mbuga tunazojivunia kuwa na wanyamapori wengi zinakabiliwa na hatari ya kutoweka iwapo watu wanaoishi kandokando ya maeneo hayo hawataacha tabia mbaya za kuwauua wanyama hao.
“Wanyamapori wengi wanauawa bila kibali. Wakati mwingine watu wanataka kupata nyama, wakati mwingine wauaji wanachukua sehemu tu kama pembe za ndovu na faru na kuacha nyama ioze. Lazima tulinde wanyamapori wetu,” alisema gwiji huyo wa siasa barani Afrika.
Kwa kuelewa umuhimu wa sekta hii ya ufahidhi, Serikali ya Tanzania, kupitia Wizara yake ya Maliasili na Utalii, na taasisi zilizo chini yake kama vile Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), imekuwa mstari wa mbele kuimarisha ulinzi na uhifadhi wa wanyamapori katika hifadhi zake zake zote zipatazo 21.
Juhudi hizi za uhifadhi ndizo zilizozaa wimbi la ujio wa watalii nchini katika miaka ya hivi karibuni, na kukuza sekta hiyo kupitia kwa wawekezaji wa ndani na wa nje.
Maono ya Mwalimu Nyerere ya kulinda raslimali za taifa ambazo Mwenyezi Mungu alizikabidhi kwa Tanzania yamekuwa ni chemichemi ya maendeleo ya kiuchumi tunayoyashuhudia katika sekta ya uhifadhi leo. Bado tunahitaji kuongeza jitihada zaidi kutunza urithi wa hifadhi zetu.
Chanzo: Gazeti la Sauti ya Mara
No comments:
Post a Comment