NEWS

Wednesday, 14 October 2026

Uwanja wa Gofu Serengeti wakamilika kwa asilimia 100



Kamishna wa Uhifadhi wa TANAPA, Massana Mwishawa, akizungumza na waandishi wa habari leo Oktoba 14, 2026 kuhusu uzinduzi ujao wa Uwanja wa Gofu Hifadhi ya Taifa Serengeti. Kulia ni Msimamizi wa ujenzi wa uwanja huo, Mhandisi Enock Magile.

Na Mwandishi Wetu
Serengeti
----------------

Uwanja wa Gofu ambao umejengwa pembezoni mwa Hifadhi ya Taifa Serengeti katika eneo la Fort Ikoma umekamilika kwa asilimia 100, Kamishna wa Uhifadhi wa Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Massana Gibril Mwishawa amesema.

Kwa mujibu wa Kamishna Mwishawa, uwanja huo wenye hadhi ya kimataifa utazinduliwa na kuanza kutumika rasmi Oktoba 18, 2026 katika hafla itakayoshuhudia makumi ya wachezaji wa gofu wabobezi kutoka mataifa mbalimbali.

“Wachezaji 81 kutoka Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda na Malawi watashiriki katika mechi za gofu wakati wa hafla ya uzinduzi wa uwanja huu, hatua inayotarajiwa kukuza mchezo huo na kuitangaza Hifadhi ya Serengeti kama kivutio kinachounganisha michezo na utalii wa asili.

“Uwanja huu ni miongoni mwa viwanja bora vya gofu vya kimataifa, na upekee wake ni kwamba wachezaji watakuwa wanacheza huku wakitazama wanyamapori wa aina mbalimbali,” Kamishna Mwishawa amesema leo Oktoba 14, 2026 katika mkutano na waandishi wa habari ndani ya uwanja huo.

Amesema mgeni rasmi katika uzinduzi wa uwanja huo unaojulikana kama Serengeti National Park Golf Course, anatarajiwa kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Ashatu Kijaji, kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Uwanja huo wa kimkakati ambao umejengwa kwenye eneo lenye ukubwa wa ekari 450, ulibuniwa na TANAPA kama sehemu ya mazao mapya ya utalii, ili kuongeza vionjo na thamani ya vivutio vya Hifadhi ya Serengeti, lakini pia kuimarisha nafasi ya Tanzania katika masoko ya kimataifa.

Aidha, Kamishna Mwishawa amesema uwanja huo utapanua shughuli za kufurahisha wageni, kuongeza muda wa kukaa kwao katika Hifadhi ya Serengeti, mapori ya akiba ya Ikorongo- Grumeti na Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori ya Ikona, na hivyo kuimarisha fursa za mapato yatokanayo na utalii.

Kamishna Mwishawa akicheza gofu kwenye Uwanja wa Gofu Hifadhi ya Taifa Serengeti leo Oktoba 14, 2026. (Picha zote na Mara Online News)

“Uwanja huu unatarajiwa kuwavutia wapenzi wa gofu na watalii wa ndani na nje ya Tanzania, sambamba na kufungua fursa za ajira, biashara, usafiri, malazi, chakula na huduma nyingine kwa jamii zinazozunguka hifadhi.

“Huu ni uwanja ambao unalenga kuongeza pato la taifa na kuboresha maisha ya jamii,” amesema Kamishna Mwishawa.

Ameongeza “Watalii wakiongeza siku za kukaa Serengeti, tutavuna mapato zaidi kwa ajili ya maendeleo ya taifa.”

Amesema utekelezaji wa mradi huo ulizinduliwa rasmi na Bodi ya Wadhamini ya TANAPA, Desemba 2022 chini ya uenyekiti wa Jenerali George Marwa Waitara, Mkuu wa Majeshi Mstaafu.

Hifadhi ya Taifa Serengeti inatembelewa na maelfu ya wageni kutoka kona mbalimbali za dunia na imekuwa ikishinda Tuzo za Hifadhi Bora Afrika mara kwa mara.

Pia, hifadhi hiyo inasifika kwa kuwa makundi ya nyumbu wahamao na wanyamapori wengine wengi, wakiwemo ‘Big Five’.

Hivyo, Mwishawa amesema uwepo wa uwanja huo wa gofu utaongeza mvuto wa hifadhi hiyo, kupanua masoko ya utalii na kuchochea fursa za kiuchumi, huku irithi wa asili wa taifa ukiendelea kulindwa kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Kwa upande wake, Msimamizi wa ujenzi wa uwanja huo, Mhandisi Enock Magile, ambaye pia ni mtaalamu wa gofu, amesema tayari umetambuliwa na kuidhinishwa na Vyama vya Gofu Duniani kwa ajili ya kutumika.

“Uwanja huu wa gofu una hadhi ya kimataifa na huduma zote zinazohitajika kwa ajili ya wachezaji wa gofu kutoka maeneo mbalimbali duniani,” amesema.

Kwa mujibu wa Mhandisi Magile, mashindano yote kwenye uwanja huo yatakuwa yanarushwa mbashara (live) na kuonekana kote duniani.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages