NEWS

Friday, 16 October 2026

Viongozi wa wananchi, wahifadhi watarajia makubwa fursa za uchumi Uwanja wa Gofu Serengeti



Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Angelina Marco, akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake leo Oktoba 16, 2026 kuhusu fursa za kiuchumi zitakazofunguliwa na Uwanja wa Gofu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa katika wilaya hiyo.

Na Christopher Gamaina
Serengeti
------------------

Viongozi wa wananchi wilayani Serengeti na wahifadhi kutoka Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) wameonesha matumaini makubwa kuhusu fursa za kiuchumi zinazotarajiwa kufunguliwa na Uwanja wa Gofu uliojengwa pembezoni mwa Hifadhi ya Taifa Serengeti katika eneo la Fort Ikoma.

Wamesema mradi huo, pamoja na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa unaotarajiwa kujengwa katika wilaya hiyo, vitaongeza idadi ya watalii, ajira, wigo wa biashara na kuinua uchumi wa jamii, mapato ya TANAPA na serikali kutokana na shughuli za utalii na mchezo wa gofu.

Wameeleza hayo kwa nyakati tofauti leo Oktoba 16, 2026 katika mazungumzo na waandishi wa habari waliotembelea uwanja huo wa gofu na vijiji vilivyo jirani.

“Uwanja wa Gofu Serengeti utachangia kushawishi watalii wengi kutoka maeneo mbalimbali duniani kuja kucheza gofu na kufanya utalii wa wanyamapori,” amesema Mkuu wa Wilaya (DC) ya Serengeti, Angelina Marco.

DC Angelina ameongeza kuwa uwanja huo wa gofu ni fursa itakayounganisha utalii wa wanyamapori na michezo kwa kuwavutia wageni wanaotafuta uzoefu unaojumuisha burudani na mandhari ya asili.

Matarajio yake mengine ni kwamba uwanja huo wa gofu na ujenzi ujao wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Serengeti vitachochea shughuli mbalimbali za kiuchumi, kuanzia huduma za malazi na usafiri hadi biashara za bidhaa, vyakula na burudani za kitamaduni.

Aidha, wafanyabiashara wadogo na wajasiriamali wanatarajiwa kunufaika kwa kuuza bidhaa zinazohitajiwa na watalii, zikiwemo vyakula, vinywaji, bidhaa za asili na kazi za mikono.

“Wana-Serengeti tumefurahi sana, uwanja huu wa gofu pamoja na uwanja wa ndege utakaojengwa katika wilaya yetu vitatusogeza karibu zaidi na watalii,” amesema Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Park Nyigoti, Mtiro Marinya.

Mwenyekiti Mtiro akizungumza na waandishi wa habari kijijini Park Nyigoti kuhusu namna watakavyonufaika na Uwanja wa Gofu Serengeti

Mtiro amesema fedha zitakazotokana na ununuzi wa bidhaa na huduma kutoka kwa wananchi zitaongeza mzunguko wa fedha katika jamii, kuimarisha biashara na kuinua kipato cha familia na kaya.

Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Robanda, Yohana Mzalendo, naye amesema uwanja huo wa gofu pia ni fursa itakayounganisha uhifadhi, utalii na maendeleo ya kiuchumi ya wananchi wanaoishi jirani na eneo hilo.

“Huu ni mradi wa kihistoria ambao utakuwa chachu ya maendeleo yetu, lakini pia ni fursa ambayo tutaitumia kutangaza kikundi cha ngoma yetu ya asili ya Waikoma iitwayo Ghahenya,” amesema Mzalendo.

Mwenyekiti Mzalendo akizungumza na waandishi wa habari mbele ya jengo la ofisi yake kijijini Robanda

Mmoja wa wasanii wa kikundi cha ngoma ya asili ya Ghahenya, Msami Maro, amesema tayari wamejipanga kutumia utajiri wao wa kitamaduni kama sehemu ya bidhaa za utalii zinazoweza kuwavutia wageni.

Msami amesema ngoma za asili, muziki, sanaa za mikono, mavazi ya kitamaduni na maonesho yanayoakisi historia na maisha ya jamii za eneo hilo ni miongoni mwa fursa zinazoweza kuendelezwa.

Amesema vikundi vya utamaduni vitaweza kujipatia mapato kwa kutoa burudani na maonesho kwa wageni wanaotembelea eneo hilo, huku vikichangia kutangaza urithi wa kitamaduni wa Serengeti.

“Tunatarajia kunufaika na uwanja wa gofu uliojengwa na TANAPA, kwa sababu sisi kama wanakikundi tunatarajia kuingiza mapato kutokana na burudani za asili kwa watalii na wachezaji watakaokuja kucheza gofu,” amesema Msami.

Kikundi cha ngoma ya asili ya Waikoma cha Ghahenya kikionesha umahiri wake wa kutoa burudani mbele ya waandishi wa habari waliotembelea kijijini Robanda leo

Kwa upande wake Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi wa TANAPA, Godwell Ole Meing’ataki, amesema manufaa ya uwanja wa Gofu Serengeti ni pamoja na kuimarisha mahusiano na jamii inayopakana na Hifadhi ya Taifa Serengeti.

Amesisitiza kuwa wananchi ni wadau muhimu wa TANAPA na kwamba wamekuwa wakiwashirikisha kwa kuwapa elimu kuhusu umuhimu na faida za uhifadhi, lakini pia kuwapa fursa za kutembelea hifadhi na kujua tabia za wanyamapori.

“Pia, kupitia idara yetu ya Ujirani Mwema tumekuwa tukitekeleza miradi ambayo imeacha alama kwa jamii zinazozunguka hifadhi zetu, kama vile shule, maji, afya, barabara, vituo vya polisi, miradi ya kufuga nyuki na kukopeshana,” amesema Meing'ataki.

Mhifadhi Meing'ataki akizungumza na waandishi wa habari katika Uwanja wa Gofu Serengeti

Mhifadhi Meing'ataki ameongeza kuwa shughuli za utalii na mchezo wa gofu zitachochea upatikanaji wa ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja, hasa kwa vijana na wanawake wanaoishi katika vijiji vinavyozunguka eneo hilo.

Ajira hizo zinaweza kujumuisha kazi za ukarimu hotelini, upishi, usafi, usafirishaji, uongozaji watalii, huduma za wageni na shughuli za uendeshaji na utunzaji wa miundombinu inayohusiana na utalii na mchezo wa gofu.

Kwa wananchi wenye mitaji na uwezo wa kuwekeza, amesema fursa zinaweza kupatikana katika ujenzi na uendeshaji wa hoteli, nyumba za kulala wageni, migahawa, kampuni za usafiri na biashara nyingine zitakazohitajika kuhudumia wageni.

Naye Mhifadhi Abedi Mwesigwa kutoka Kitengo cha Mahusiano ya Jamii Hifadhi ya Taifa Serengeti, amesema uwanja huo wa gofu utakuwa zao jingine la utalii litakaloongeza pato ambalo sehemu yake itapelekwa kwenye jamii kugharimia utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Amesema mafanikio ya matarajio hayo yanahitaji ushirikiano na mahusiano ya karibu kati ya mamlaka za uhifadhi, jamii, serikali na wawekezaji ili kuhakikisha shughuli za kiuchumi haziathiri mazingira, wanyamapori na mifumo ya ikolojia inayoifanya Serengeti kuwa eneo muhimu la utalii wa kiwango cha kimataifa.

“Hatuna Hifadhi ya Taifa Serengeti bila mahusiano na jamii. Hifadhi hii inazungukwa na wilaya nane, ambazo ni Serengeti, Bunda, Tarime, Busega, Meatu, Bariadi, Itilima na Ngorongoro.

“Uhifadhi sasa hivi unatoka kwenye kutumia nguvu kwenda kwenye kutumia wananchi. Jamii ikielewa umuhimu wa hifadhi na wanyamapori ndiyo inaweza kushiriki kuilinda,” amesema Mhifadhi Mwesigwa.

Mhifadhi Mwesigwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu umuhimu wa kushirikisha jamii katika ulinzi wa wanyamapori

Kwa mujibu wa Mhifadhi Mwesigwa, mkoa wa Mara pekee umenufaika na shilingi bilioni 25.4 kutoka TANAPA kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo ya jamii ndani ya kipindi cha miaka mitano kuanzia 2021.

Inaelezwa kwamba wageni watakaokwenda kucheza gofu huku wakifurahia kutazama wanyamapori na mandhari ya Hifadhi ya Taifa Serengeti watashawishika kuongeza muda wa kukaa eneo hilo, na hivyo kuongeza pia matumizi ya huduma zinazotolewa na wananchi na wafanyabiashara wa ndani.

Vilevile, inatarajiwa kwamba Uwanja wa Gofu Serengeti utaongeza mvuto wa eneo hilo kwa soko la kimataifa la watalii wanaopenda michezo, burudani na uzoefu wa kipekee wa mazingira ya asili.

Kamishna Mwishawa akicheza gofu kwenye Uwanja wa Gofu Serengeti. (Picha zote na Mara Online News)

Utalii unaohusisha mchezo wa gofu pia unaweza kuvutia kundi jingine la wageni wenye mahitaji mbalimbali ya huduma, wakiwemo wachezaji wa gofu, familia zao na watu wanaosafiri kwa ajili ya mapumziko na burudani.

Hali hiyo itashawishi uongezaji wa mahitaji ya huduma za hoteli, nyumba za kulala wageni, migahawa, usafiri, waongoza watalii, kufua nguo, bidhaa za matumizi binafsi na huduma nyingine zinazohitajiwa na wageni.

Lakini pia, wazalishaji wa bidhaa za mikono na wajasiriamali wa ndani wanaweza kuanzisha au kuboresha bidhaa zinazolenga soko la wageni, kwa kuzingatia ubora, ubunifu, bei zinazokubalika na mahitaji ya soko la utalii.

Hivyo, wahifadhi na viongozi wa wananchi wamewataka wakazi wa vijiji vinavyopakana na Uwanja wa Gofu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Serengeti, pamoja na wajasiriamali kutoka maeneo mengine wilayani kujipanga mapema ili kunufaika na fursa zinazoweza kufunguliwa na miradi hiyo.

Sambamba na hayo, vijana na wanawake wanahimizwa kutafuta mafunzo katika maeneo ya ukarimu, lugha za kigeni, ujasiriamali, usimamizi wa biashara na huduma kwa wateja ili kuongeza ushindani wao katika soko la ajira na huduma za utalii.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages