NEWS

Sunday, 18 October 2026

Waziri Kijaji azindua Uwanja wa Gofu Serengeti, asema TANAPA ni mfano wa kuigwa



Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Ashatu Kijaji, akicheza gofu leo Oktoba 18, 2026 katika hafla ya uzinduzi rasmi wa uwanja wa gofu uliojengwa na TANAPA pembezoni mwa Hifadhi ya Taifa Serengeti katika eneo la Fort Ikoma.

Na Mwandishi Wetu
Serengeti
------------------

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Ashatu Kijaji, amelipongeza Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) kwa kujenga Uwanja wa Gofu Serengeti akisema utakuwa na maana kubwa katika kuongeza mapato ya utalii kwa maendeleo ya taifa.

Waziri Kiijaji ameyasema hayo leo Oktoba 18, 2026 katika hafla ya uzinduzi rasmi wa uwanja huo wa gofu ambao umejengwa pembezoni mwa Hifadhi ya Taifa Serengeti katika eneo la Fort Ikoma.

“TANAPA wameonesha mfano halisi wa namna ya kusimamia na kutumia rasilimali vizuri.,” amesema Waziri Kijaji ambaye alikuwa mgeni rasmi katika uziduzi wa uwanja huo kwa niaba ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Amesema uzinduzi rasmi wa uwanja huo wa gofu ni tukio la kihistoria katika ukuaji wa sekta ya utalii, hususan utalii wa michezo nchini na kwamba Tanzania iko tayari kuwa mwenyeji wa mashindano ya michezo ya gofu Afrika na duniani kwa ujumla.

Hivyo, ameiagiza Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) kuingiza uwanja huo kwenye orodha ya vifurushi vya utalii inavyovitangaza katika maeneo mbalimbali duniani.

"Ujenzi wa uwanja huu ni mkakati wa serikali wa kuifanya Tanzania isiwe tu kitovu cha utalii wa wanyamapori, bali pia iwe kitovu cha utalii wa michezo," amesema.

Amesema uwanja huo wa gofu utaongeza ajira mpya na kuchochea maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi.

Waziri huyo amesema utalii wa michezo unakua kwa kasi kubwa duniani, hivyo Tanzania haiwezi kuwa nyuma katika kutumia fursa hiyo kuingiza mapato yanatotokana na sekta hiyo.

Ameongeza kuwa utawavutia watalii na wacheza gofu wa kimataifa ambapo watakuwa wanacheza huku wakifurahia kutazama wanyamapori.

Waziri Kijaji akikata utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa uwanja huo wa gofu

Aidha, Waziri Kijaji amewakaribisha wawekezaji wa huduma mbalimbali za kitalii na kuahakikishia ushirikiano wa kutosha kutoka Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Samia.

Kwa upande wake Kamishna wa Uhifadhi wa TANAPA, Massana Mwishawa, amesema ujenzi wa uwanja huo umekidhi ubora na viwango vya kimataifa.

“Ni matarajio yetu kuwa uwanja huu utakuwa na maana kubwa kiuchumi na kukuza vipaji vya mchezo wa gofu,” Kamishna Mwishawa amesema katika taarifa yake kwa mgeni rasmi.

“Huu ni uwanja ambao una vigezo na viwango vya kimataifa, tutautunza na kuendelea kuuboresha zaidi ili uongeze mapato kwa maendeleo ya taifa,” ameongeza.

Lengo la uwanja huo ni kuongeza vionjo kwa watalii ambao wanazuru katika Hifadhi ya Taifa Serengeti kutoka maeneo mbalimbali duniani ili waweze kukaa zaidi katika eneo hilo.

Upekee wa uwanja huo ni kwamba unatoa fursa adimu kwa watalii kucheza gofu huku wakitazama aina mbalimbali za wanyamapori ambao ni kivutio kikiubwa katika hifadhi hiyo.

Kamishna Mwishwa pia amewashukuru watangulizi wake (makmishna wa uhifadhi wastaafu) kwa maono yao kuhusu mradi huo ambao sasa umekamilika kwa asilimia 100.

Waziri Kijaji akiweka jiwe la msingi la uwanja huo wa gofu. (Picha zote na Mara Online News)

Hafla ya uzinduzi huo imehudhuriwa pia na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Rhimo Nyansaho, Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbas, Wakuu wa Wilaya, Wabunge na wadau mbalimbali wa utalii na uhifadhi.

Viongozi wengine waliohudhuria hafla ya uzinduzi wa uwanja huo wa gofu ni pamoja na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Patrick Chandi Marwa, Mkuu wa mkoa huo, Brigedia Jenerali Evans Mtambi na Mbunge wa Jimbo la Serengeti, Mery Daniel Surati.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages