
Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba akizungumza na wananchi (hawapo pichani) katika mkutano wa hadhara uliofanyika Nyamuswa, Bunda mkoani Mara jana Ijumaa.
Bunda
-------------
Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba ameagiza hatua kali zichukuliwe dhidi ya walioshindwa kutimiza wajibu wao hadi kusababisha majengo ya Hospitali ya Wilaya ya Bunda kutitia.
Dkt. Mwigulu alitoa agizo hilo jana Ijumaa, wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika Nyamuswa, Bunda mkoani Mara, baada ya kukagua ujenzi wa hospitali hiyo.
“Nimeambiwa Waziri wa Afya alishatengeneza timu na ikafanya kazi na TAKUKURU. Nizipate taarifa hizo ili hawa waliofanya makosa haya wawajibike kule kule walipo, lazima wawajibike,” alisema.
Wakati wa ukaguzi huo Waziri Mkuu alikuta majengo mawili yametitia na kupewa maelezo kwamba hali hiyo imesababishwa na uwepo wa chanzo cha maji na udongo mfinyanzi.
“Nauliza kwanini majengo yametitia wanasema ni kwa sababu yamejengwa karibu na chanzo cha maji. Chanzo cha maji kimekuja baada ya kujenga? Si kilikuwepo pale pale. Wanasema udongo huu ni wa mfinyanzi, kwani hawakuujua?
“Haya ni mambo ya aibu. Unawezaje kujenga jengo la kituo cha afya kwenye eneo linalotitia. Hii haikubaliki, lazima tuchukue hatua kali. Waziri ikithibitika hawa msiwahamishwe wafukuzwe,” alisisitiza Dkt. Mwigulu.
Aidha, alisema serikali itaendelea kufuatilia suala hilo ili kubaini ukweli wa kilichosababisha majengo hayo kutitia, huku ikihakikisha wananchi hawapati adhabu kutokana na uzembe katika utekelezaji wa miradi ya serikali.
“Tumeongea na Mkuu wa Mkoa, Mbunge na Katibu Tawala, tutatafuta hizo fedha ili kukamilisha, wananchi wetu wasipate adhabu kwa ajili ya uzembe wa waliopewa jukumu hilo ambao hawakutimiza wajibu wao,” alisema.
Awali, Mbunge wa Jimbo la Bunda Vijijini, Boniphace Mwita Getere, alimdokeza Waziri Mkuu kwamba ujenzi wa hospitali hiyo ambao hata hivyo haujakamilika, umekadiriwa kugharimu hadi shilingi bilioni saba.
Ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Bunda ulianza Mei 2019. Hadi sasa, serikali imeshatoa shilingi bilioni 5.39 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo.
Hospitali hiyo imeanza kutoa huduma mbalimbali, zikiwemo za wagonjwa wa nje, kulaza wagonjwa, maabara, afya ya uzazi na mtoto, kujifungua, radiolojia, macho na meno.

Waziri Mkuu Mwigulu akisalimiana na viongozi mbalimbali wa chama na serikali wakati alipowasili Bunda.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu Mwigulu amesema serikali imechukua hatua mbalimbali kukabiliana na kupanda kwa bei ya saruji, ikiwemo kuelekeza uondoaji kodi kwenye malighafi inayotumika katika uzalishaji wa saruji, yaani klinka.
“Nimewaelekeza Mamlaka ya Mapato [TRA] waondoe kodi kwenye klinka ili upatikanaji wa saruji uwe wa uhakika na bei iweze kuwa himilivu,” alisema.
Kuhusu huduma za afya, Dkt. Mwigulu alisisitiza kuwa wananchi hawapaswi kuchangishwa fedha za mafuta kwa ajili ya magari ya serikali, hususan ya wagonjwa yanayotumika kuokoa maisha.
“Hatuwezi tukawa na magari ya serikali yana mafuta, halafu ambulance ya kunusuru maisha ya wagonjwa tuchangishane mafuta. Haya ni mambo ya mazoea ambayo hatutaki kuwa utaratibu wa serikali,” a;lisema.
Waziri Mkuu Mwigulu pia alisisitiza umuhimu wa wagonjwa walio katika hali mbaya kupewa huduma ya dharura haraka kabla ya kukamilisha taratibu nyingine za kiutawala.
“Mgonjwa aliyezidiwa amefika, hatua ya kwanza apelekwe moja kwa moja kwenye kitanda apate huduma. Hata kumwandikisha mtamwandikisha akiwa ameshapata huduma ya kwanza. Kanusuru kwanza maisha yake. Usifanye itifaki kwenye maisha,” alisisitiza.
Kuhusu upatikanaji wa dawa, Dkt. Mwigulu alisema serikali imeendelea kutoa fedha kwa ajili ya ununuzi wa dawa na vifaa tiba, hivyo akuwataka viongozi na watendaji wa afya kuhakikisha vinawafikia wananchi waliokusudiwa.
Waziri Mkuu Mwigulu alikuwa katika ziara ya siku mbili Bunda kukamilisha ziara yake ya kukagua miradi ya maendeleo na kusikiliza kero za wananchi mkoani Mara aliyoifanya Julai mwaka huu.
No comments:
Post a Comment