
Mwenyekiti wa ALAT Mkoa wa Mara, Ayub Mwita Makuruma, akizungumza katika kikao cha jumuiya hiyo kwenye ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Novemba 13, 2026.
Tarime
-------------


-------------
Jumuiya ya Serikali za Mitaa Tanzania (ALAT) Mkoa wa Mara imezitaka halmashauri za mkoa huo kuendelea kuzingatia utoaji wa asilimia 10 ya fedha za mapato ya ndani kwa ajili ya mikopo isiyo na riba kwa makundi ya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu.
Mwenyekiti wa ALAT Mkoa wa Mara, Ayub Mwita Makuruma, amesisitiza hayo leo Novemba 14, 2026 katika kikao cha jumuiya hiyo cha majumuisho ya taarifa za ukaguzi wa miradi ya maendeleo katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime.
"Tuendelee kusimamia fedha za asilimia kumi, kuhakikisha watu wanapata mikopo ili kujiletea maendeleo, lakini pia kurudisha kwa ajili ya wengine.
"Tunamshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuruhusu hizi fedha kwa makundi hayo pamoja na bilioni zaidi ya mia nne kwa miradi ya maendeleo, na tayari robo tatu imeishatekelezwa,” alisema Makuruma ambaye pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti.

Sehemu ya wajumbe wa ALAT Mkoa wa Mara kikaoni
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Matera Newland Chacha, aliahidi kuwa maelekezo waliyopewa na ALAT yatafanyiwa kazi kwenye miradi yote iliyotembelewa, ikiwemo elimu, barabara na maji.
'Tutatekeleza maagizo yote mliyotupatia, ikiwemo urasimishaji wa maeneo ya shule, kukamilika kwa miradi inayoaksi thamani ya fedha,” alisema Chacha.
Awali, wajumbe wa ALAT Mkoa wa Mara wakiongozwa na Makuruma waliipongeza halmashauri hiyo kwa utekelezaji wa miradi ya mbalimbali ya maendeleo inayoaksi thamani ya fedha zilizotumika.

Mwenyekiti wa ALAT Mkoa wa Mara, Ayub Mwita Makuruma (kushoto aliyevaa shati jeupe), akiongoza wajumbe wa jumuiya hiyo kukagua miradi ya maendeleo katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime.
Muonekano wa mbele wa majengo ya Shule ya Msingi mpya ya Maika
Miradi mingine iliyotekelezwa ni kuzibua na kulima barabara katika kata ya Nyamwaga zenye urefu wa kilomita 3.1 pamoja na ujenzi wa makalavati 11 kwa gharama ya shilingi milioni 486.
Pia, ujenzi wa vyoo vya nje, kichomea taka na matenki mawili ya kuvunia maji ya mvua kwa gharama ya shilingi milioni 65.
Mwingine ni ujenzi wa nyumba ya mtumishi katika Shule ya Msingi Nyarero uliogharimu shilingi milioni 54 baada ya wananchi kukamilisha ujenzi wa boma sawa na thamani ya shilingi milioni 24, huku halmashauri ikichangia shilingi milioni 30 za mapato ya ndani.
Mwenyekiti wa ALAT Mkoa wa Mara, Ayub Mwita Makuruma, akikabidhi shilingi milioni moja kupiga jeki ujenzi wa nyumba ya mtumishi wa Shule ya Msingi Nyarero katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime. (Picha zote na Mara Online News)


No comments:
Post a Comment