
Meneja Mkuu wa Mgodi wa Dhahabu wa North Mara, Stephen Doyle (aliyevaa bukta ya kijivu na viatu vyeusi), Meneja Mahusiano wa mgodi huo, Francis Uhadi (kushoto kwa Doyle) na Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele (kushoto kwa Uhadi), wakijiandaa kuongoza mbio fupi wakati wa uzinduzi wa Wiki ya Mahusiano leo Novemba 14, 2026 katika mji wa Nyamongo.
Tarime
-------------
Mgodi wa Dhahabu wa North Mara umezindua Wiki ya Mahusiano leo Jumamosi, Novemba 14, 2026 ili kuendeleza na kuimarisha ujirani mwema na wananchi wa vijiji vinavyouzunguka.
Hatua hiyo ni mwendelezo wa mpango wa mgodi huo uliokuwa ukifahamika awali kama Kombe la Mahusiano (Mahusiano Cup).
“Leo sio tu kwamba tunakimbia lakini pia tunasherekea alama ya mahusiano ya muda mrefu tuliyonayo na jamii,“ Meneja Mkuu wa mgodi huo, Stephen Doyle, amesema wakati wa hafla ya uzinduzi huo ambao umefanyika katika viwanja vya Shule ya Sekondari Ingwe, wilayani Tarime.

Wakifanya zoezi la kuhitimbisha mbio
Uzinduzi huo umetanguliwa na mbio fupi ambazo zimehusisha makundi mbalimbali, wakiwemo wafanyakazi wa mgodi huo, maafisa wa serikali na viongozi wa kijamii kutoka vijiji jirani.
Mgodi huo ambao unazungukwa na vijiji 11 vinavyonufaika na uwekezaji huo, unaendeshwa na kampuni ya Barrick kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia kampuni ya Twiga Minerals.
Doyle amesema mgodi huo utaendelea kuwekeza kwenye miradi ya maendeleo endelevu katika vijiji hivyo kupitia mpango wake wa Uwajibikaji kwa Jamii (CSR).
Hata hivyo, ametumia fursa hiyo pia kuomba kumalizika kwa tatizo la vitendo vya uvamizi katika mgodi huo, akisema vinaweza kuathiri uzalishaji wake wa dhahabu na maendeleo ya jamii.
Meneja Mkuu wa Mgodi, Stephen Doyle akizungumza katika hafla ya uzinduzi huo.
Aidha, Meneja Mkuu huyo amesema ahadi ya kampuni Barrick ya kujenga uwanja wa kisasa wa michezo katika vijiji vinavyozunguka mgodi huo iko mbioni kuanza kutekelezwa.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele, amesema mahusiano mema ni muhimu kwa ajili ya uwekezaji na maendeleo endelevu katika vijiji vilivyo jirani na mgodi huo.
“Tukivamia mgodi tunarudisha nyuma uzalishaji. Maeneo yaliyo jirani na mgodi huu yamepiga hatua kubwa ya maendeleo. Tutumie vizuri mibaraka hii,” amesema Meja Gowele ambaye alikuwa mgeni ramsi katika uzinduzi huo.

Mkuu wa Wilaya, Meja Edward Gowele, akizungumza katika hafla hiyo.
Mkuu huyo wa Wilaya amesisitiza kuwa kila upande, yaani wananchi na mgodi huo lazima utekeleze wajibu wake kwa ustawi wa pande zote.
Amepongeza kazi nzuri inayofanywa na ofisi ya mahusiano ya mgodi huo katika kutatua changamoto zinazojitokeza na kuimarisha mahusiano na jamii inayouzunguka.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Maendeleo ya Jamii (CDC) katika Mgodi wa North Mara, Rashid Bogomba, amesema wiki hiyo ya mahusiano itahusisha pia mikutano ya kuongea na wananchi wa vijiji 11 vilivyo jirani na mgodi huo kuhusu umuhimu wa kudumisha mahusiano mema na kampuni ya Barrick.
Mwenyekiti wa CDC, Rashid Bogomba.
Bogomba pia amesisitiza umuhumu wa jamii kushirikiana kukemea vitendo vya wavamizi katika mgodi huo.
“Tutafute namna ya kumaliza tatizo la ‘intrusions’ ili tuendelee kunufaika na fedha za CSR zinazotolewa na mgodi,” amesema Bogomba.
Mgodi huo umekuwa ukitenga wastani wa shilingi bilioni nne kila mwaka kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya jamii kupitia mpango wa CSR.
Taarifa zilizopo zinaonesha kuwa mgodi huo umewekeza shilingi zaidi ya bilioni 30 kwenye miradi mbalimbali ya maendeleo ya jamii katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime kupitia mpango wake wa CSR tangu 2019 ulipokabidhiwa kwa kampuni ya Barrick hadi sasa.


No comments:
Post a Comment