
Meneja Mkuu wa Mgodi wa Dhahabu wa North Mara, Stephen Doyle, akimvisha mchezaji medali baada ya mechi ya kirafiki ya Nyamongo FC na Giant FC katika hafla ya kilele cha Wiki ya Mahusiano iliyofanyika Nyamongo wilayani Tarime, jana Jumapili.
Tarime
-----------
Mamlaka wilayani Tarime zimeonya kuwa watu wanaovamia Mgodi wa Dhahabu wa North Mara kuiba mawe ya dhahabu hawatavumiliwa, hivyo kuwataka kuacha vitendo hivyo mara moja.
“Suala la uvamizi wa mgodi halikubaliki hata kidogo, wale wanaiojiita ‘intruders’ ni majambazi,” Katibu Tawala wa Wilaya (DAS) ya Tarime, Sauli Mwaisenye alionya jana Jumapili.
DAS Mwaisenye alitoa onyo hilo wakati akizungumza katika kilele cha Wiki ya Mahusiano iliyoandaliwa na mgodi huo kuendeleza na kuimarisha ujirani mwema na wakazi wa vijiji vinavyouzunguka.
Hafla hiyo ilifanyika katika viwanja vya Shule ya Sekondari Ingwe, ambapo pia ilipambwa na mechi ya kirafiki ya timu za soka Nyamonga FC na Giant FC.
Mwaisenye ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya, Meja Edward Gowele, aliupongeza mgodi huo kwa juhudi unazofanya katika kuimarisha mahusiano mazuri na jamii inayouzunguka.
Mbali na kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, kiongozi huyo alisistiza kuwa uwekezaji wa mgodi huo ambao unaendeshwa na kampuni ya Barrick kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia kampuni ya Twiga Minerals una manufaa makubwa kwa taifa.

DAS Mwaisenye akizungumza katika hafla hiyo
Kwa upande wake Meneja Mkuu (GM) wa mgodi huo, Stephen Doyle, alisema vitendo vya uvamizi na uharibifu wa miundombinu ya mgodi unahatarisha maisha ya watu, kukwamisha uzalishaji wa dhahabu na kupunguza mapato ya serikali na fedha za miradi ya Uwajibikaji kwa Jamii (CSR).
“Ninatoa wito kwa vijana wetu, wazazi na viongozi kulinda amani na kutumia njia zetu za wazi za mawasiliano na utatuzi wa malalamiko,” GM Doyle alisema.
Alibainisha kuwa mgodi huo umewekeza shilingi bilioni 31 kati ya mwaka 2019 na 2025 kutekeleza miradi 253 katika maeneo ya elimu, afya, maji, mazingira na mindombinu kupitia mpango wake wa CSR.
Aidha, alisema maandalizi ujenzi wa miradi ya kimkakati, ukiwemo wa soko la dhahabu Nyamongo na kituo cha mabasi Nyamwaga yanaendelea, huku mradi mkubwa wa maji ambao kwa sasa unatoa huduma katika vijiji vitano ukiwa umeshakamilika.
GM Doyle aliongeza kuwa mgodi huo pia unashirikiana na Kamati yake ya Maendeleo ya Jamii (CDC) kufanya maandalizi ya kuanza ujenzi wa uwanja wa kisasa wa michezo ambao utanufaisha vijiji vyote 11 vinavyouzunguka.

GM Doyle akielezea namna Mgodi wa Dhahabu wa North Mara unavyochangia maendeleo ya jamii
Kwa mujibu wa GM huyo, katika siku nane za Wiki ya Mahusiiano, mgodi huo ulivifikia vijiji vyote 11 na kufanya mazungumzo ya moja kwa moja na wananchi kupitia mijadala ya wazi ambayo iliambatana na burudani za kitamaduni.
Pia, masuala ya kiusalama yalipewa umuhimu katika wiki hiyo ya mahusiano.
“Programu hii ya Mahusiano imeendelea kuwa daraja muhimu katika kujenga uaminifu, umoja na kuishi kwa amani kati ya Mgodi wa Dhahabu wa North Mara na jamii zinazotuzunguka,” alisema.
Hafla hiyo ilihuduriwa na viongozi mbalimbali, akiwemo Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini, Mwita Waitara, madiwani na viongozi wa vijiji 11 vinavyozunguka mgodi huo.

Mbunge Waitara akikabidhi zawadi kwa mwakilishi wa washindi wa mechi hiyo ya kirafiki
Waitara alisema mgodi huo umetekeleza miradi mingi ambayo inasaidia kuharakisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika vijiji vinavyouzunguka.
“Mgodi umesaidia maeneo mengi, huu mradi wa maji ni wa CSR kutoka mgodini, barabra hii ya lami hapa Nyamongo ni CSR na kuna shilingi milioni 800 ambazo zimetengwa kujenga soko la dhahabu Nyamongo ni kutoka CSR. Lakini pia kuna shule mpya za msingi na sekondari zimejengwa hapa,” alisema mbunge huyo.
Naye Diwani wa Kata ya Kemambo, Rashid Bogomba, alisema uzalishaji ukiongezeka katika mgodi huo unakuwa na faida nyingi kwa jamii inayouzunguka na taifa kwa ujumla.
“Tukizalisha zaidi na sisi tunapata gawio zaidi kama nchi, lakini pia na sisi wananchi tunaozunguka eneo hili la mgodi tunaendelea kunufaika kupitia fedha za CSR,” alisema Bogomba ambaye pia ni Mwenyekiti wa CDC.
Hafla hiyo ya kilele cha Wiki ya Mahusiano ilihitimishwa kwa mshindi wa mechi ya kirafiki, Giant FC, kukabidhiwa zawadi ya kombe na fedha taslimu baada ya kuichapa Nyamongo FC kwa mikwaju ya penati 4-3.

Viongozi wakikabidhi kombe la ushindi kwa Nahodha wa Giant FC
Kaulimbiu ya Wiki ya Mahusiano inasema "Mahusiano Bora kwa Uwekezaji Endelevu".
No comments:
Post a Comment