
Wadau wa Programu ya ASILIB wakifurahia picha ya pamoja wakati wa kikao chao kilichoandaliwa na MVIWANYA na kufanyika Novemba 17, 2026 mjini Tarime.
Tarime
--------------
Mtandao wa Vikundi vya Wakulima na Wafugaji Nyancha (MVIWANYA) umewakutanisha wadau mbalimbali kutathmini shughuli za kilimo mseto zilizofanyika kwa mwaka kupitia Programu ya ASILIB - CC 2026-2028.
Shuguli hizo zinazofadhiliwa na Shirika la Vi Agroforestry na kutekelezwa na MVIWANYA katika wilaya za Serengeti na Tarime, mkoani Mara.
Kikao hicho kilifanyika Novemba 17, 2026, mjini Tarime, ambapo kilihudhuriwa na wajumbe wa Bodi ya MVIWANYA, wakulima, wafugaji, maafisa kilimo, mazingira, maendeleo ya jamii na walimu wa shule za msingi na sekondari.

Kikao kikiendelea mjini Tarime
Lengo la kikao hicho lilikuwa kutathmini mafanikio, walichojifunza, changamota na kuweka mikakati ya kuzitatua katika utekelezaji wa mradi huo kwa mwaka ujao.
Kwa mujibu wa Mratibu wa MVIWANYA, Joel Nguvava, mradi huo umepata mafanikio makubwa ambayo yamechangiwa na mwitikio mzuri kutoka kwa wakulima.

Mratibu wa MVIWANYA, Joel Nguvava, akizungumza katika kikao hicho.
"Tumefanikiwa kwa kutekeleza malengo kwa asilimia zaidi ya 80, wakulima kujiongezea kipato kwa asilimia 85, uzalishaji wa mazao ya biashara na chakula.
"Kwenye suala la kuhifadhi mazingira tumeweza kupanda miti laki moja na elfu nane, ikiwemo ya matunda,” alisema Nguvava.

Wakuu wa shule zilizotekeleza vizuri Programu ya ASILIB walipewa zawadi kwa ajili ya shule zao wakati wa kikao hicho.
"Wito wangu, serikali, wadau wa sekta binafsi na wakulima tushirikiane ili kuhamasisha jamii iweze kuzalisha kwa tija na kupata kipato endelevu,” Mratibu Nguvava.
Kwa upande wao wakuu wa idara za kilimo, mifugo na uvuvi waliipongeza MVIWANYA kwa ushirikiano inaoutoa katika kuhamasisha na kuwezesha vikundi vya wakulima.
"Ushirikiano na MVIWANYA umesaidia sana kwenye idara ya kilimo kwenye usalama wa chakula, kusaidia, kuwezesha vikundi vya kilimo na kuziba pengo pale ambapo serikali haifiki,” alisema Mkuu Idara ya Kilimo Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Peregia Joel Balozi.
Naye Mkuu wa Idara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi Wilaya ya Serengeti, Ismael Bayinga, alisema Programu ya ASILIB imekuwa na matokeo chanya kwa wafugaji na wakulima.

Makabidhiano ya zawadi kwa wakuu wa shule yakiendelea. (Picha zote na Mara Online News)
"Tumeona matokeo, wafugaji wanafuga kwa tija, wanauza mayai na kuku, wakulima wanazalisha mazao ya bustani kujiongezea kipato, kujikimu na kupeleka watoto shule, lakini pia upandaji miti katika shule za msingi na sekondari.
"Ushirikiano unaoendelezwa vizuri ukihusisha wataalamu wa ugani kwenye vijiji, kata na wilaya umetoa matokeo mazuri,” alisema Bayinga.
No comments:
Post a Comment