NEWS

Wednesday, 25 November 2026

Rais Samia agawanya wizara mbili, apangua Mawaziri, Makatibu Wakuu



Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan

Na Mwandishi Wetu
--------------------------

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amefanya mabadiliko ya muundo wa wizara mbili, uteuzi na uhamisho wa viongozi mbalimbali ili kuimarisha utendaji wa serikali.

Kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa jana na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Dkt. Moses Kusiluka, Rais Samia amegawanya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushiriano wa Afrika Mashariki kuwa wizara mbili.

Wizara hizo mpya ni Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Halikadhalika, Mkuu huyo wa nchi amegawanya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuwa wizara mbili; ambazo ni Wizara ya Mifugo na Wizara ya Uvuvi.

Kufuatia mabadiliko hayo, Rais Samia amemteua Balozi Mahmoud Thabit Kombo kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, huku Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki akiteuliwa kuwa Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Wengine walioteuliwa kuwa mawaziri na wizara zao zikiwa kwenye mabano ni Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa (Mifugo), Hamis Mohamed Mwinjuma (Uvuvi), David Ernest Silinde (Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi) na Beng’i Mazana Issa (Mawasiliano na Teknolojia ya Habari).

Walioteuliwa kuwa Naibu Mawaziri ni Dkt. Ngwaru Jumanne Maghembe (Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa) na James Kinyasi Millya (Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki).

Wengine walioteuliwa kuwa Naibu Mawaziri ni Subira Khamis Ngalu (Wizara ya Uvuvi) na Cecilia Daniel Paresso (Wizara ya Kilimo).

Wakati huo huo, Rais Samia amemteua Agnes Meena kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Prof. Mohammed Ali Sheikh kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Uvuvi.

Aidha, Rais amemhamisha Eliakim Chacha Maswi kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwenda kuwa Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).

Naye Gerson Partinus Msigwa amehamishwa kutoka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwenda kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsi, Wanawake na Makundi Maalum.

Kwa upande mwingine, Rais Dkt. Samia amemteua Dkt. Ayub Rioba Chacha kuwa Mkurugenzi wa Idara ya Habari – Maelezo na Msemaji Mkuu wa Serikali.

Uapisho wa Mawaziri, Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu wateule utafanyika tarehe itakayopangwa baadaye, kwa mujibu wa taarifa hiyo iliyosainiwa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Bakari Machumu.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages