NEWS

Wednesday, 25 November 2026

Maandalizi ujenzi Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Serengeti yafikia pazuri



Mbunge wa Jimbo la Serengeti, Mary Daniel Surati.

Na Mwandishi Wetu
Serengeti
--------------

Maandalizi ya ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Serengeti yamefikia hatua ya kuhakikisha watu wanaopisha mradi huo wanalipwa fidia.

Kwa mujibu wa Mbunge wa jimbo la Serengeti, Mary Daniel Surati, hatua hiyo ni muhimu kuekelea ujenzi wa uwanja huo ambao umesubiriwa kwa miaka zaidi ya 20 sasa.

“Sasa hivi tupo katika hatua ya kuhakikisha kuwa wananchi wetu ambao wameridhia kupisha ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Serengeti wanaenda kupewa malipo yao ya fidia,” alisema Mary wakati akihutubia mkutano wa hadhara katika mji wa Serengeti mapema wiki hii.

Aliwataka wakazi wa Serengeti kupuuza kile alichokiita upotoshaji dhidi ya miradi mikubwa ambayo utekelezaji wake unaendelea katika jimbo hilo.

Mbunge huyo pia alidokeza kuwa eneo la ujenzi wa uwanja huo limeongezeka ili kukidhi hadhi ya viwango vya kimataifa.

“Katika kuhakikisha kwamba tunakwenda kujenga Uwanja wa Ndege wa Kimataifa ambao unakidhi viwango vya kimataifa, tumehakikisha uwanja ule unaongezwa ukubwa wake,” alisema.

Hata hivyo, hadi sasa, mamlaka husika hazijaweka hadharani idadi ya watu wanaopisha mradi huo wala kiasi cha fedha za fidia watakacholipwa.
Sehemu ya eneo lililotengwa kwa ajili ya ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Serengeti

Ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Serengeti, ambao umesuasua kwa miongo zaidi ya miwili, umetajwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya chama tawala - Chama Cha Mapinduzi ya Mwaka 2025-2030.

Lengo la ujenzi wa uwanja huo ni kuufanya mji wa Serengeti (zamani mji wa Mugumu) kuwa kitovu cha utalii kwani unapakana na hifadhi bora Afrika - Hifadhi ya Taifa Serengeti.

Ujenzi wa uwanja huo utawezesha watalii kutoka nje kutua moja kwa moja katika mji wa Serengeti na kuchochea shughuli za kiuchumi kwa wananchi wa mkoa wa Mara.

Pia, inaelezwa kuwa ujenzi wa mradi huo wa kimkakati utapunguza idadi ya ndege zinazotua ndani ya Hifadhi ya Taifa Serengeti kwa sasa.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages