
Waziri wa Maliasili na Utalii Tanzania, Dkt. Ashatu Kijaji (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi mbalimbali.
Tanzania imeendelea kuimarisha nafasi yake katika ramani ya utalii duniani baada ya kutangazwa kuwa mwenyeji wa hafla ya utoaji wa Tuzo za Dunia za Utalii (World Travel Awards – WTA) kwa mwaka 2026.
Hafla ya utoaji wa tuzo hizo itafanyika Desemba 12, 2026 katika Hifadhi ya Taifa Serengeti.
Tangazo hilolitolewa Novemba 5, 2026 na Mwanzilishi na Rais wa WTA, Graham Cooke, wakati wa hafla maalum iliyofanyika katika kilele cha Maonesho ya Kimataifa ya Utalii ya World Travel Market (WTM) jijini London, Uingereza.
Cooke alisema Tanzania imechaguliwa kutokana na upekee wake katika sekta ya utalii, akibainisha kuwa Serengeti ni moja ya majina makubwa yanayotambulika barani Afrika na duniani kutokana na utajiri wake wa wanyamapori na vivutio vya kipekee.
Aliongeza kuwa uwepo wa Mlima Kilimanjaro, ambao ni mrefu zaidi barani Afrika, pamoja na uzuri wa vivutio vya asili na ukarimu wa Watanzania, ni miongoni mwa sababu zilizoifanya Tanzania kuwa chaguo sahihi la kuandaa tukio hilo la kimataifa.
Kwa upande wake, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Ashatu Kijaji, alimshukuru Cooke na taasisi ya WTA kwa kuichagua Tanzania kuwa mwenyeji wa hafla hiyo muhimu.
Dkt. Ashatu alisema serikali ipo tayari kuhakikisha wageni kutoka sehemu mbalimbali duniani wanapata uzoefu wa kipekee wa utalii wa Tanzania.
Alisema Serengeti nayo ipo tayari kupokea wageni zaidi ya 500 wanaotarajiwa kuhudhuria hafla hiyo kutoka mataifa mbalimbali duniani.
Aidha, alisema tukio hilo ni fursa muhimu ya kuitangaza Tanzania, kuongeza muonekano wake kimataifa na kuimarisha nafasi yake katika soko la utalii duniani.
Dkt. Kijaji alitumia nafasi hiyo pia kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa juhudi na uongozi wake katika kuifungua Tanzania na kuimarisha diplomasia.
Alisema kazi kubwa inayofanyika chini ya uongozi wa Rais Samia imechangia kwa kiasi kikubwa kuitangaza Tanzania na kuiweka katika nafasi nzuri zaidi katika jukwaa la kimataifa la utalii.
Hafla hiyo ilihudhuriwa pia na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbas na Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Dkt. Thereza Mugobi.
No comments:
Post a Comment