NEWS

Sunday, 29 November 2026

Umemejua kunufaisha wakazi wa visiwani Musoma Vijijini



Mojawapo ya mifumo ya nishati ya umemejua katika jimbo la Musoma Vijijini

Na Mwandishi Wetu
Musoma
--------------

Juhudi za kusambaza nishati ya umemejua (solar energy) zinaendelea katika visiwa vyenye wakazi vilivyopo kata za Etaro, Kiriba na Makojo katika jimbo la Musoma Vijijini, mkoani Mara.

Katika taarifa yake kwa Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Musoma wiki hii, Mbunge wa jimbo hilo, Prof. Sospeter Muhongo, alisema umemejua unatarajiwa kuwa kichocheo kikubwa cha maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika visiwa hivyo.

Prof. Muhongo alisema umemejua ni sawa na umeme unaozalishwa na gesi asilia, maji, mafuta, makaa ya mawe na jotoardhi, hivyo wananchi wanapaswa kuuona kama fursa muhimu ya maendeleo.

Akitoa mfano wa mafanikio ya matumizi ya umemejua duniani, Prof. Muhongo alisema China na India ni miongoni mwa nchi zinazozalisha nishati hiyo kwa wingi na kuitumia kuendesha uchumi wenye ushindani.

Alisema kisiwa cha Rukuba kilichopo kata ya Etaro ni miongoni mwa maeneo ya jimbo la Musoma Vijijini yanayonufaika na matumizi ya umemejua.

Kisiwa cha Rukuba kina uzoefu wa matumizi ya umemejua kwani tayari Wakala wa Umeme Vijijini (REA) imeweka nishati hiyo katika Kituo cha Afya cha kisiwa hicho.

Mbali na huduma za afya, umemejua unatarajiwa kuwa na mchango mkubwa katika utekelezaji wa mradi wa maji ya bomba kisiwani Rukuba.

Prof. Muhongo alisema Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) ina mpango wa kuweka miundombinu ya usambazaji wa maji ya bomba katika kisiwa hicho, ambapo umemejua utahitajika kuyasambaza kwa wananchi.

Hata hivyo, mbunge huyo alieleza kutoridhishwa na kasi ya utekelezaji wa miradi ya umemejua katika visiwa hivyo. “Miradi ya umemejua kwenye visiwa hivyo inaenda polepole mno,” alisema.

Kutokana na hali hiyo, Prof. Muhongo aliwataka viongozi wa kata za Etaro, Kiriba na Makojo kuendela kuhamasisha wakazi wa visiwa hivyo ili washawishike kuweka umemejua katika maeneo yao ya makazi na biashara.

Aliongeza kuwa matumizi ya nishati hiyo yanapaswa kupanuliwa hadi kwenye shule, miradi ya maji ya bomba na huduma nyingine muhimu zinazohitaji umeme wa uhakika.

Pamoja na changamoto ya kasi ya utekelezaji, Prof. Muhongo aliipongeza REA) kwa kuendelea kutekeleza majukumu yake vizuri katika jimbo la Musoma Vijijini.

“REA inaendelea kufanya kazi nzuri, ikiwemo utekelezaji wa miradi ya umemejua kwenye visiwa vya jimbo letu,” alisema.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages