
Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele, akizungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Oktoba 27, 2026 katika kata ya Nyanungu inayopakana na Hifadhi ya Taifa Serengeti. (Picha na Sauti ya Mara)
------------------------------------------
HATIMAYE ukurasa mpya wa kurejesha ushirikiano na ujirani mwema kati ya Hifadhi ya Taifa Serengeti na vijiji vinavyopakana nayo upande wa wilaya ya Tarime mkoani Mara umefunguliwa.
Katika hatua hiyo, pande zote mbili zimezingatia ukweli kwamba uhifadhi endelevu wa wanyamapori hauwezi kutegemea sheria na doria pekee, bali unahitaji pia ushiriki wa jamii ambayo haiachwi nyuma katika kunufaika na rasilimali hizo.
Tembo wanapoingia mashambani kuharibu mazao ya wakulima, wafugaji wanapokosa maji na malisho ya mifugo, huku vijana wakikosa fursa za ajira na biashara hifadhini, dhana ya uhifadhi inakosa nguvu kwa jamii zinazoishi jirani na maeneo yaliyohifadhiwa.
Kwa muda mrefu, wakazi wa vijiji vinavyopakana na Hifadhi ya Taifa Serengeti upande wa Tarime, wamekuwa wakikabiliana na changamoto zinazogusa maslahi ya pande zote, zikiwemo za mpaka, usalama, matumizi ya ardhi na upatikanaji wa fursa za kiuchumi.
Hata hivyo, hatua ya makubaliano ya kurejesha ushirikiano na ujirani mwema baina ya pande hizo mbili, ni mwanzo mzuri wa safari ya kuunganisha uhifadhi na maendeleo ya jamii.
Makubaliano hayo yalifikiwa Oktoba 27 na 28, 2026 katika mikutano ya hadhara iliyoongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele, katika vijiji mbalimbali vya kata za Nyanungu, Gorong’a na Kwihancha.
Katika majadiliano, wananchi hao walilalamikia kero ya tembo wanaoingia mashambani na kuharibu mazao, hali inayowasababishia umaskini katika familia na wakati mwingine kuhatarisha maisha yao.
Wanataka changamoto zao zitatuliwe ili mafanikio ya uhifadhi yaendane na ulinzi wao dhidi ya athari za wanyamapori wakali na waharibifu.
“Sisi wananchi tuko tayari kwa mahusiano na ujirani mwema, lakini tunaomba hifadhi itusaidie kuboresha huduma za kijamii, vijana wetu wapewe nafazi za ajira hifadhini na wahifadhi wadhibiti tembo wanaotuvamia vijijini,” anasema mkazi wa Gorong’a, Anatory Chacha.
Chacha anasisitiza kuwa wananchi hawapingi uhifadhi, bali wanahitaji kuona umuhimu wake katika maisha yao. “Tunataka kuwa sehemu ya mafanikio ya uhifadhi badala ya kuwa watazamaji tu,” anasema.
Wanataja changamoto nyingine kuwa ni upungufu wa maeneo ya malisho na vyanzo vya maji kwa mifugo, unaowalazimu baadhi ya wafugaji kuingia ndani ya hifadhi kutafuta maji na malisho.
Mkazi wa kijiji cha Gibaso katani Kwihancha, Marwa Mhagachi, anaeleza kuwa baadhi ya wananchi wamekuwa wakilazimika kupeleka mifugo kunywa maji ndani ya hifadhi kutokana na ukosefu wa malambo katika maeneo yao.
Matokeo yake, anasema wafugaji wamekuwa wakiishia kukamatwa na kutozwa faini, jambo linalozidisha malalamiko na mvutano na mamlaka za hifadhi.
“Wananchi wanalazimika kwenda kunywesha mifugo maji ndani ya hifadhi kutokana na ukosefu wa malambo katika maeneo yetu,” anasema Mhagachi.
Ujenzi wa malambo, uboreshaji wa vyanzo vya maji na mipango ya matumizi ya ardhi ni hatua zinazoweza kupunguza shinikizo la mifugo kuingia maeneo yaliyohifadhiwa.
Ajira na biashara
Kwa upande mwingine, wakazi wa vijiji hivyo wameeleza kutoridhishwa na ukosefu wa fursa za ajira na biashara zinazopatikana ndani ya Hifadhi ya Serengeti.
Kutokana na hali hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Tarime ameielekeza Hifadhi ya Serengeti kuwapa wakazi wa vijiji hivyo fursa za ajira, zikiwemo za muda mfupi na biashara zinazohitajika ndani ya hifadhi.
“Vijana na wanawake kutoka vijiji hivi wapewe kipaumbele cha kazi, zikiwemo za muda mfupi na biashara zinazohitajika hifadhini, ili waweze kujikwamua kiuchumi,” anasema Meja Gowele.
Anasema wanakijiji wanapopata ajira katika shughuli za hifadhi, wanapopewa nafasi ya kusambaza bidhaa na kushiriki katika mnyororo wa thamani wa utalii, hifadhi inakuwa sehemu ya fursa za kiuchumi kwa jamii.
Hata hivyo, Mkuu wa Wilaya amewataka wananchi wanaopata ajira, zikiwemo kazi za muda mfupi hifadhini kuwa waaminifu na waadilifu kwenye mali za hifadhi na watalii. “Vijana mnaopata ajira muwe waaminifu ili kujijengea imani kwa hifadhi,” anasisitiza.
Kwa mujibu wa Afisa Mahusiano ya Jamii wa Hifadhi ya Taifa Serengeti, Mhifadhi Abed Mwesigwa, Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) linaendelea kutenga fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo ya jamii zinazozunguka hifadhi.
Akijibu hoja za wananchi hao, Mkuu wa Kanda ya Kaskazini Serengeti, Mhifadhi Ezron Lema, amewataka kutoa taarifa wanapobaini tembo wanaovamia vijiji au wanapokutana na askari wanaodaiwa kutokuwa waadilifu ili hatua stahiki zichukuliwe.
Kwa upande wake Mkuu wa Ulinzi wa Hifadhi ya Taifa Serengeti, Elisamehe Ayubu, anasema ujangili ukipungua, TANAPA itaelekeza fedha ambazo zingetumika kugharimia shughuli za ulinzi kwenye miradi ya jamii.
Kwa tafsiri nyingine, kadiri ushirikiano unavyoimarika na uhalifu kupungua, ndivyo nafasi ya kuelekeza rasilimali zaidi kwenye maendeleo ya jamii inavyoweza kuongezeka.

Mhifadhi Ayubu akizungumza kwenye mkutano wa hadhara kijijini Gibaso
Mikutano endelevu
Moja ya maazimio ya mikutano hiyo ni agizo la Mkuu wa Wilaya kuitaka Hifadhi ya Serengeti kuhakikisha inakutana na wakazi wa vijiji hivyo kila baada ya miezi mitatu ili kujadili changamoto, hatua zilizochukuliwa, kutathmini utekelezaji wa makubaliano na kugawana majukumu.
Kuhusu mvutano wa mpaka kati ya vijiji na Hifadhi ya Serengeti, Mkuu wa Wilaya amewataka wananchi kuwa watulivu na wavumilivu wakati wakisubiri maelekezo ya viongozi wa ngazi za juu serikalini.
Kwa mujibu wa kiongozi huyo, masuala ya mipaka yanapohusisha maslahi ya jamii na rasilimali za taifa, yanahitaji maamuzi yenye ushahidi, uwazi na kuzingatia taratibu za kisheria.
Hifadhi ya Taifa Serengeti ni rasilimali muhimu kwa taifa na urithi wa asili wenye thamani kubwa kwa dunia. Hata hivyo, mafanikio ya kuilinda hayawezi kutenganishwa na maisha ya wananchi wanaoizunguka.
Mkuu wa Wilaya anasisitiza umuhimu wa wananchi hao kuimarishiwa huduma za maji, elimu, afya, barabara, upatikanaji wa ajira na mazingira salama ya kuzalisha mali.
“Lengo letu tunataka muishi kwa kushirikiana na kutegemeana, muwe na mahusiano mazuri. Hatutaki watu waishi kwa manung’uniko ndani ya nchi yao,” anasisitiza Meja Gowele.
Anasema hifadhi haiwezi kuwa imara kwa muda mrefu ikiwa jamii inayoizunguka inaishi katika mazingira ya malalamiko na ukosefu wa fursa za maendeleo.
Hivyo, mafanikio ya makubaliano hayo yatapimwa kwa mabadiliko yatakayoonekana katika maisha ya wanavijiji hao na usalama wa rasilimali za Hifadhi ya Serengeti.
Tembo watakapozuiwa kuleta madhara kwa wanavijiji, vijana watakapopata ajira, wafugaji watakapopata malambo ya maji nje ya hifadhi, haki za wananchi zitakapoheshimiwa na wao kushiriki katika kulinda hifadhi, ndipo maana halisi ya ujirani mwema itakapodhihirika.
Chanzo: Gazeti la Sauti ya Mara
No comments:
Post a Comment