NEWS

Sunday, 1 November 2026

Mradi wa CSR Barrick: Wananchi 150 Kewanja waomba kuunganishiwa huduma ya maji ya bomba kwenye makazi yao



Sehemu ya vituo vya kuchotea maji vya mradi mkubwa wa maji ya bomba uliotekelzewa kutokana na fedha za CSR Barrick North Mara ili kuboresha upatikanaji wa huduma ya maji kwa wakazi wa vijiji vilivyo jirani na mgodi huo. (Picha ya Maktaba)

Na Mwandishi Wetu
Tarime
-------------

Wananchi takriban 150 katika kijiji cha Kewanja kilichopo Nyamongo wilayani Tarime, wameomba kuunganishiwa huduma ya maji ya bomba kwenye makazi yao, kufuatia uzinduzi wa upanuzi wa mradi wa maji kijijini hapo.

Mradi huo ambao ulizinduliwa hivi karibuni na Mkuu wa Wilaya hiyo, Meja Edward Gowele, umegharimiwa na Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara kupitia mpango wake wa Uwajibikaji kwa Jamii (CSR).

Kwa mujibu wa Kaimu Meneja wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Tarime, Mhandisi Mohamed Mtopa, usambazaji wa huduma ya maji kwa wananchi wa eneo hilo unaendelea vizuri.

“Usambazaji wa huduma ya maji unaendelea vizuri na hadi sasa tayari wananchi 150 wameomba kuunganishiwa huduma ya maji ya bomba majumbani mwao,” Mhandisi Mtopa ameiambia Sauti ya Mara kwa njia ya simu leo Jumapili.

Amesema upanuzi wa mradi huo umewezesha wananchi takriban 30,000 kufikiwa na huduma ya maji safi na salama ya bomba katika vijiji vya Kewanja, Matongo, Nyabichune, Mjini Kati na Nyangoto vilivyopo jirani na mgodi huo.

Mhandisi Mtopa ameendelea kutoa wito kwa wananchi wa maeneo hayo kuthamini, kutunza na kulinda miundombinu ya mradi huo wa maji ili uweze kudumu muda mrefu kwa manufaa yao na vizazi vijavyo.

Upanuzi wa mradi huo ni sehemu ya jitihada za kuboresha huduma za kijamii katika maeneo yanayozunguka mgodi huo ambao unaendeshwa na kampuni ya Barrick kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia kampuni ya Twiga Minerals.

Chanzo: Gazeti la Sauti ya Mara

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages