NEWS

Friday 29 May 2020

Maswa wajenga kiwanda cha viazi lishe


HALMASHAURI ya Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu, imekamilisha ujenzi wa kiwanda cha viazi lishe kitakachozalisha ajira kwa wananchi na kuwahakikishia wakulima soko la zao hilo.

Pia kiwanda hicho kitasaidia kuipunguzia halmashauri hiyo utegemezi wa mapato kutoka Serikali Kuu.
Profesa Riziki Shemdoe (kulia waliosimama katikati) na Dkt Fredrick Sagamiko katika ukaguzi wa shughuli za kiwanda cha viazi lishe wilayani Maswa.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Dkt Fredrick Sagamiko, ujenzi wa kiwanda hicho umegharimu Sh milioni 461 na kwamba kina uwezo wa kukausha viazi vyenye uzito wa tani 1.5  kwa siku.

Dkt Sagamiko amesema hay oleo Mei 29, 2020 wakati akisoma taarifa ya ujenzi wa kiwanda hicho mbele ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Profesa Riziki Shemdoe.

Hata hivyo, Dkt Sagamiko amesema kiwanda hicho cha viazi lishe kinakabiliwa na uhaba wa fedha za uendeshaji.

Katika hotuba yake, Katibu Mkuu, Profesa Shemdoe, ameeleza kuridhishwa na uwekezaji huo na kutumia nafasi hiyo kutoa mwito kwa halmashauri nyingine nchini kuja kujifunza Maswa.
Baadhi ya wafanyakazi wa kiwanda cha viazi lishe wilayani Maswa wakiwa kazini 
Aidha, Profesa Shemdoe ameliagiza Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda Tanzania (TIRDO) kupeleka haraka nishati mbadala kiwandani hapo ili kuongeza uzalishaji.

Tayari kiwanda hicho kimepata soko la unga lishe unaotumika kutengeneza vyakula mbalimbali katika mikoa ya Singida, Iringa, Dodoma, Shinyanga na Mara.

(Imeandikwa na Anita Balingilaki, Maswa)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages