NEWS

Saturday 6 June 2020

Walinda amani wanawake toka Brazil, India walivyotwaa tuzo ya jinsia ya UN 2019


MWANAMKE mlinda amani kutoka Brazil anayehudumu nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati na mlinda amani mwanamke kutoka India ambaye amehitimisha hivi karibuni jukumu lake nchini Sudan Kusini, wamechaguliwa kupokea Tuzo ya Mwaka 2019 ya Umoja wa Mataifa (UN) ya mwanajeshi mchagizaji wa masuala ya kijinsia.

Washindi hao, Kamanda Carla Monteiro de Castro Araujo, Afisa wa Jeshi la Anga la Brazili ambaye kwa sasa anahudumu kwenye mpango wa Umoja wa Matafa wa kurejesha utulivu nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati (MINUSCA) na Meja Suman Gawani kutoka Jeshi la India, mwanajeshi mwangalizi wa zamani wa mpango wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini (UNMISS), walipokea tuzo hiyo wakati wa hafla iliypfanyika mtandaoni ikiendeshwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika kuadhiisha Siku ya Kimatafa ya Walinda Amani Ijumaa Mei 29, mwaka huu.
Tuzo ya Jinsia ya UN
Tuzo hiyo “Mwanajeshi mchagizaji wa mwaka wa masuala ya kijinsia” iliyoanzishwa mwaka 2016, inatambua kujitolea na juhudi za mwanajeshi mlinda amani katika kuchagiza misingi ya azimio namba 1325 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu wanawake, amani na ulasalma katika muktadha wa operesheni za amni, wakipendekezwa na wakuu au makamanda wa operesheni za ulinzi wa amani.

Kwa mara ya kwanza, wanawake hao walinda amani walipokea tuzo hiyo kwa pamoja kwa mchango wao katika suala hilo muhimu.

Baada ya kupokea taarifa za ushindi huo, Kamanda Monteoro de Castro Araujo alisema Tuzo hii ni utambuzi wa kazi inayohusisha kikosi cha MINUSCA na kitengo cha raia. Ni jambo la kufurahisha na kuridhisha kwangu mimi na kwa mpango mzima kuona kwamba miradi yetu inazaa matunda.
Naye Meja Gawani alielezea faraja yake kwa kuona kazi yake kama askari mwangalizi wa Umoja wa Mataifa imetambuliwa.
“Kwa majukumu yetu yoyote, msimamo wetu au cheo chetu ni jukumu letu kama walinda amani kujumuisha mtazamo wa jinsia zote katika kazi yetu ya kila siku na kuumiliki, katika muingiliano na wafanyakazi wenzetu, pamoja pia na jamii,” alisema Meja Gawani.
Kamanda Monteiro
Kamanda Monteiro de Castro Araujo amehudumu kama mwanajeshi mshauri wa jinsia na ulinzi katika vikosi vya MINUSCA makao makuu tangu Aprili 2019.

Wakati wa muhula wake alianzisha na kuendesha mafunzo ya kina katika masuala yanayohusiana na jinsia na ulinzi.

Kupitia juhudi zake, mpango huo uliongeza kwa kiasi kikubwa idadi ya wasimamizi wa masuala ya jinsia na ulinzi na vituo pia.

Pia alikuwa chachu muhimu katika kushuhudia doria za hatua zinazohusisha masuala ya jinsia zikihusisha jamii na kukiongezeka kutoka 574 hadi kufikia karibu 3,000 kwa mwezi.
Meja Gawani
Tangu kupelekwa kwake UNMISS Desemba 2018, Meja Gawani amefundisha waangalizi zaidi ya 230 wa Jeshi la Umoja wa Mataifa (UNMO) kuhusu ukatili wa kingono unaohusiana na vita na kuhakikisha uwepo wa waangalizi wanajeshi wanawake katika kila timu ya vituo vya mpango huo.

Kwa kutoa msaada, ushauri, mwongozo na uongozi, Meja Gawani alisaidia kuunda mazingira ya kuwezesha walinda amani wa Umoja wa Mataifa.

Pia alifundisha vikosi vya Serikali ya Sudan Kusini na kuwasaidia kuzindua mpango mkakati wao wa kukabiliana na ukatili wa kingono uliohusiana na vita.
Hongera kwa kazi nzuri
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, aliwapongeza Kamanda Monteiro de Castro Araujo na Meja Gawani kwa tuzo zao.
“Walinda amani hawa ni mfano wa kuigwa, kupitia kazi zao wameleta mitazamo mipya na wamesaidia kujenga imani na ujasiri katika jamii tunazozitumikia.” alisema Katibu Mkuu huyo na kuongeza:
“Kupitia kujitolea na njia zao za ubunifu wamekumbatia kiwango cha ubora ambacho ni msukumo mkubwa kwa walinda amani wote kila mahali. Tunapokabiliana na changamoto za sasa kazi yao haijawahi kufaa au kuwa na umuhimu zaidi kama wakati huu.”

Huu ni mwaka wa pili mfululizo mlinda amani kutoka Brazil anapokea tuzo hiyo ya heshima na ni mara ya kwanza tuzo hii kwenda kwa mlinda amani kutoka India.



Washindi wa Tuzo ya Masuala ya Jinsia ya UN Mwaka 2019, Meja Suman Gawani (Kushoto) wa Jeshi la India aliyetumika awali UNMISS na Kaman Carla Monteiro de Castro Araujo, Afisa wa Jeshi la Anga la Brazil ambaye sasa anafanyakazi na MINUSCA.



No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages