NEWS

Wednesday 5 August 2020

Kambi za uhamilishaji sasa ni kila kona nchini

Ng'ombe wakiwa bandani kwa ajili ya uhamilishaji

KAIMU Mkurugenzi Msaidizi wa uendeshaji vinasaba vya mifugo na uzalishaji, Abdallah Temba, amesema Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi imeanzisha kambi za teknolojia mpya ya uhimilishaji ili kuwafikia wafugaji nchini kote.

 

Temba ameyasema hayo Agosti 4, 2020 wakati akizungumza na waandishi wa habari katika maonesho ya Nanenane yanayofanyika kitaifa kwenye viwanja vya Nyakabindi wilayani Bariadi, Simiyu.

 

Amesema kambi hizo zinahusisha wataalamu kutoka wizarani na kituo cha taifa cha uhimilishaji ambapo wamekuwa wakitoa mafunzo ya teknolojia hiyo kwa wataalamu walioko mikoani na kwenye halmashauri.

 

Temba ameongeza kuwa wizara imeleta teknolojia hiyo kwa wafugaji ili kukuza tija kwenye mifugo kutokana na ng'ombe waliopo nchini kutokuwa na uwezo wa kuzalisha mazao ya maziwa na nyama kwa wingi.

 

“Ili kuboresha mazao yatokanayo na mifugo, tumekuja na teknolojia ya uhimilishaji kwa njia ya chupa ambapo katika kituo chetu cha taifa cha uhimilishaji mifugo kwa njia ya chupa (NAIC) kilichopo jijini Arusha kuna madume bora yanayoweza kutoa mbegu za aina mbalimbali na teknolojia hii imeenezwa nchi nzima,” amesema. 

 

Aidha, Temba amesema serikali imeboresha maabara iliyoko Arusha ikilinganishwa na maabara zilizoko kanda ya Afrika Mashariki na Kati na kwamba mbegu zinazotoka kwenye maabara hiyo ni bora na zinaweza kuuzwa nje ya nchi.

 

Temba ametumia nafasi hiyo kuwahimiza wafugaji nchini kupeleka mifugo yao kwenye maonesho ya Nanenane yanayofanyika kwenye kanda zote nchini, ambapo uhimilishaji unafanyika bure.

 

Kwa upande wao, wafugaji akiwemo Nashon Jirabi kutoka Butiama mkoani Mara na Sarapia Kulwa kutoka wilaya ya Maswa mkoani Simiyu, wamesema uhimilishaji umewasaidia kufuga kwa tija na kuongeza kipato, huku ndama wanaozaliwa kwa njia hiyo wakionekana wenye afya.

 

(Imeandikwa na Anita Balingilaki, Bariadi)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages