NEWS

Wednesday 5 August 2020

Nduhiye ahimiza wafanyabiashara kusajili biashara, kampuni zao

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Ludovick Nduhiye (kulia) akizungumza na wafanyakazi wa Brella kwenye maonesho ya Nanenane Nyakabindi wilayani Bariadi, Simiyu.

NAIBU Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Ludovick Nduhiye, amewataka wafanyabiashara kusajili majina ya biashara na kampuni zao ili kutambulika na kuchochea ukuaji wa uchumi wao na taifa kwa jumla.

Mbali na hilo, Nduhiye amesema awali kulikuwa na shughuli na biashara zisizo rasmi nchini, lakini kwa sasa shughuli nyingi na biashara zimerasimishwa.

"kusajili na kurasimisha biashara, pato la taifa linaongezeka, unapofanya mahesabu (kukokotoa) kuhusu mgawanyo /wastani wa pato la mwananchi wa kawaida uzalishaji katika taifa unapanda juu, kwa hiyo Brella wanafanya shughuli ya urasimishaji ambayo ni nyenzo muhimu sana ya kiuchumi katika kupata taarifa za uchumi kwenye taifa lolote,” amesema.

Nduhiye ameyasema hayo Agosti 2, 2020 wakati akitembelea mabanda ya Wizara ya Viwanda na Biashara kwenye  maonesho ya Nanenane yanayofanyika kitaifa katika viwanja vya Nyakabindi wilayani Bariadi, Simiyu.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Dkt Yusuph Ngenya, amesema wanawezesha wafanyabiashara hususan wadogo kushindana kwenye soko kwani kupitia alama ya ubora, bidhaa zao zinashindana kitaifa na kimataifa na kuuzwa kirahisi.

Msaidizi wa Usajili Mwandamizi, Gabriel Girangay, amesema kwa sasa wanatoa huduma ya usajili wa majina ya biashara na kampuni kwa kutumia kompyuta ambapo huduma hiyo inapatikana kwenye mtandao kwa saa 24 tofauti na zamani ambapo mteja (mfanyabiashara) alilazimika kwenda nje ya mkoa wake kufuata huduma ya usajili wa biashara/ kampuni yake.

Girangay ameongeza kuwa ni vema wananchi hususan wenye biashara na kampuni ambazo hawajasajili biashara /kampuni zao kutumia fursa ya maonesho hayo ambapo amesema usajili unafanyika papo kwa papo.

Nao baadhi ya wananchi waliotembelea maonesho hayo wamekiri kuwa yana manufaa makubwa kwao na kutoa wito kwa ambao hawajafika kujitokeza kwa wingi kupata huduma mbalimbali.


(Imeandikwa na Anita Balingilaki, Bariadi)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages