Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka akizungumza na baadhi ya wanafunzi watakaofanya mtihani wa taifa wa kuhitimu darasa la saba mkoani humo. |
MKUU
wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka ametangaza zawadi kwa wanafunzi watakaofanya
vizuri kwenye mtihani mtihani wa taifa wa kuhitimu darasa la saba utakaoanza nchini
kote kesho Jumatano.
Mbali na wanafunzi pia Mtaka ametangaza zawadi kwa walimu, shule na wilaya
ambazo zitaingia kumi bora kitaifa katika mtihani huo ambao unatarajiwa
kufanyika Oktoba 7 na 8, 2020.
"Mkoa umeandaa shilingi milioni tano zawadi kwa wanafunzi watakaofanya
vizuri kwenye mtihani huo na kuingia 10 bora kitaifa ambapo kila mwanafunzi
atapatiwa Sh. 500,000 na mbali na hilo kwa walimu mkoa umeandaa zawadi pia, mwalimu
ambaye somo lake litapata alama A nyingi atajipatia shilingi 500,000,” alisema
Mtaka.
Mtaka ameyasema hayo jana Jumatatu mbele ya wanafunzi wa darasa la saba na
walimu wa shule za msingi Sima na Somanda zilizopo Halmashauri ya Mji wa
Bariadi mkoani Simiyu wakati wa ziara yake kuangalia maandalizi kabla ya
kufanyika kwa mtihani huo.
Kuhusu shule itakayoingia kumi bora kitaifa, mkuu huyo wa mkoa
amesema itapatiwa shilingi milioni tatu, huku wilaya itayoingia 10 bora
kitaifa walimu wake watapata fursa ya kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
“Zawadi hizi ni motisha kwa walimu na wanafunzi ambazo mkoa umekuwa ukitoa kila
mwaka, katika kuhakikisha unaendelea kufanya vizuri kwenye mitihani yote na
tumefanya hivi mwaka huu kwa wanafunzi na walimu wa kidato cha sita baada ya
mkoa kushika nafasi ya tatu kitaifa… mkoa umejipanga kuhakikisha unatoa motisha
ya kutosha kwa walimu na wanafunzi.
"Niendelee kuwasisitiza viongozi wote wa mkoa kuwaheshimu walimu na
kuwatatulia changamoto zao kwa haraka, na walimu toeni taarifa kwangu kama atakuwepo kiongozi
yeyote anayewanyanyasa," amesema Mtaka.
Kwa upande wake, Afisa Elimu Mkoa wa Simiyu, Ernest Hinju amesema watahiniwa
30,779 watafanya mtihani huo mkoani humo, maandalizi yote yamekamilika na kwamba wana
uhakika kuwa lengo la mkoa kushika nafasi ya kwanza kitaifa litafikiwa.
Nao baadhi ya wanafunzi wamesema wamejipanga vyema kuhakikisha
wanashika nafasi ya kwanza kitaifa, kwani wameandaliwa vyema na walimu wao
kupitia kambi za kitaaluma.
(Imeandikwa na Anita Balingilaki, Simiyu)
No comments:
Post a Comment