NEWS

Thursday 10 December 2020

Jamii yahimizwa kuungana kupinga ukatili wa kijinsia

Kilele cha maadhimisho ya Siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia katika wilaya ya Maswa mkoani Simiyu.

 

WATOTO 148 na watu wazima 195 katika wilaya ya Maswa mkoani Simiyu wamefanyiwa ukatili ukiwemo wa kingono, kisaikolojia na biashara haramu (kwa watoto) kati ya Januari na Novemba 2020.

 

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Dwati la Jinsia Wilaya ya Maswa, WP Anande Masay, wakati wa kilele cha maadhimisho ya Siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia yaliyofanyika katika kata ya Shishiyu wilayani humo.     

Wanafunzi wakiwa katika maadhimisho hayo.

 

Aidha, WP Masay amesema kwamba katika kipindi hicho, wanafunzi 68 walipatiwa ujauzito wakiwemo 65 wa shule zsekondari na watatu wa shule ya msingi. 

 

Amesema kesi 27 zilifunguliwa mahakamani, nane zilitolewa hukumu ambapo washitakiwa walihukumiwa kifungo cha miaka kati ya 30 na maisha, tatu zilitolewa hukumu ya wahusika kuchapwa viboko, 10 zinaendelea na sita ziliondolewa mahakamani.

 

WP Masay ukatili umekuwa ukiendelea wilayani Maswa kutokana na baadhi ya ndugu kutokuwa tayari kutoa ushahidi mahakamani dhidi ya washitakiwa, jamii kuendelea kuficha matukio ya vitendo hivyo, kukosekana kwa mahabusu ya watoto na sehemu ya kuwahifadhi waathirika wa ukatili katika jeshi la polisi.

Mratibu wa Mradi wa Maendeleo ya Jamii Shishiyu kutoka World Vision Tanzania, Yohana Masanja.

 

Yohana Masanja ni Mratibu wa Mradi wa Maendeleo ya Jamii Shishiyu kutoka World Vision Tanzania ambao ni wafadhili wa maadhimisho hayo, amesema kuna haja ya kuunganisha nguvu na kubuni mikakati ya jamii itakayoleta suluhisho la kudumu.

 

Hata hivyo, Masanja amesema matunda ya mapambano dhidi ya ukatili yameanza kupatikana kutokana na ushirikishwaji wa jamii wakiwemo viongozi wa dini, mila na wazee maarufu. 

 

Ametoa wito kwa jamii nzima kuungana katika kupiga vita vitendo vya unyanyasaji, udhalilishaji na ukatili wa kijinsia ili kufikia malengo ya dira ya taifa ya mwaka 2025 inayosema "Tanzania itakuwa na jamii yenye usawa wa kijinsia ifikapo mwaka2025.” 

Wanafunzi wakifuatilia maadhimisho hayo.

 

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Katibu Tawala wa Wilaya hiyo, Agnes Alex, amewataka maofisa wa dawati la jinsia wilayani humo na wote wanaohusika kupokea taarifa za waathirika wa vitendo vya ukatili wa kijinsia kutunza siri wanazopelekewa ili jamii iwe na imani nao, hivyo kutoa taarifa zitakazosaidia kukamatwa kwa wahusika wa matukio hayo. 

 

Maadhimisho hayo yamebebwa na kaulimbiu inayosema "Tupinge ukatili wa kijinsia, mabadiliko yanaanza na mimi."

 

(Imeandikwa na Anita Balingilaki, Maswa)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages