NEWS

Monday 16 October 2023

Ubalozi wa Marekani wampongeza Gachuma kwa kuwa chachu ya mafunzo ya kuendeleza wanawake wajasiriamali



Mhe. Christopher Mwita Gachuma (wa pili kushoto) na Mratibu wa AWE Tanzania, Dkt Victoria Kisyombe (wa pili kulia) wakiwa katika picha ya pamoja na wakufunzi wa mafunzo ya AWE kwa wanawake wajasiriamali wa mkoani Mara.
----------------------------------------------

Na Waandishi Wetu, Mara
-----------------------------------


UBALOZI wa Marekani nchini Tanzania umempongeza mfanyabiashara maarufu Kanda ya Ziwa, Mhe. Christopher Mwita Gachuma, kwa kuwa chachu ya mafunzo ya kuendeleza wanawake wajasiriamali mkoani Mara, kupitia programu ya Chuo cha Wanawake Wajasiriamali (AWE). 

Mratibu wa AWE kutoka Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania, Dkt Victoria Kisyombe amewasilisha salamu hizo za pongezi kwa Mhe. Gachuma leo Jumatatu, wakati wa ufunguzi rasmi wa mafunzo ya AWE kwa wanawake wajasiriamali zaidi ya 30, yanayoendelea kwenye ukumbi wa CMG Hotel mjini Tarime, Mara.


“Mhe. mgeni rasmi [Gachuma], tunakushukuru kwa kutupatia fursa ya kulala na kuendesha mafunzo ya AWE katika hoteli yako ya CMG, huu ni moyo wa uzalendo wa hali ya juu sana. Tumepokea hisani hii kwa moyo wa shukrani na unyenyekevu. 

“Uongozi wa Ubalozi [wa Marekani nchini Tanzania] umetuma salamu nyingi kwako na kwamba umethamini mchango mkubwa uliotoa katika kuendeleza programu ya AWE mkoani Mara. 

“Na kwa heshima hii, Mhe. Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Dkt Michael Battle ameahidi kufika yeye binafsi wakati wa kufunga mafunzo haya, lakini amekuomba ukifika Dar es Salaam ufike Ubalozini ili ukutane naye,” amesema Dkt Kisyombe.
Dkt Kisyombe akiwasilisha salamu za Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania

Nao wakufunzi wa mafunzo hayo wamemtaja Mhe. Gachuma kama Mtanzania ambaye ameonesha mfano mzuri wa juhudi za kusaidia kuendeleza wanawake wajasiriamali Watanzania kupitia programu ya AWE.
Picha ya pamoja

Akifungua ramsi mafunzo hayo, Mhe. Gachuma ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama tawala - CCM, ameipongeza Serikali ya Marekani kwa kuanzisha mpango huo wa kuwezesha wanawake kiuchumi, huku akiwataka washiriki wa mafunzo hayo kutumia fursa hiyo vizuri ili kufikia ndoto zao. 

“Napenda kuushukuru Ubalozi wa Marekani kwa kuleta haya mafunzo ya AWE, jambo hili ni kubwa sana katika kuwezesha wanawake kiuchumi,” amesema Mhe. Gachuma na kuwataka washiriki wa mafunzo hayo kufanya kazi kwa bidii na uaminifu bila kukata tamaa, ili waweze kufikia mafanikio wanayoyataka. 

Mhe. Gachuma akifungua mafunzo hayo


Mhe. Gachuma akisisitiza jambo katika hotuba yake ya ufunguzi wa mafunzo hayo

Aidha, Mhe. Gachuma amewataka washiriki hao watakapohitimu mafunzo hayo kuwiwa na moyo wa kuwasaidia wengine ambao hawakubahatika kupata fursa hiyo. “Ukiwezeshwa na wewe wezesha wengine,” amesisitiza. 

Kwa mujibu Dkt Kisyombe, programu ya AWE ilianzishwa mwaka 2019 na Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani kwa ajili ya kuwasaidia wanawake wajasiriamali duniani, ikiwemo Tanzania katika juhudi za kujiinua kiuchumi. 

“Programu hii ya AWE ambayo inafadhiliwa na Serikali ya Marekani imechangia kwa kiasi kikubwa jitihada za Serikali yetu [ya Tanzania] za kuwaendeleza wanawake kiuchumi na kielimu,” amesema. 


Dkt Kisyombe amefafanua kuwa kabla ya kuanza rasmi mafunzo ya AWE, washiriki hupata kozi maalum ya Kiingereza kwa wiki mbili. 

“Kwa kifupi AWE inawapatia wanawake wajasiriamali ujuzi, zana na mitandao wanayohitaji ili kuyageuza mawazo yao kuwa biashara zenye mafanikio. Hii ni furaha kubwa kwetu kwani kumwendeleza mwanamke ni kuendeleza familia, jamii na Taifa kwa ujumla,” amesema Mratibu huyo wa AWE Tanzania. 

Amesema hadi sasa programu ya AWE nchini Tanzania imeshapata mafanikio makubwa, ikiwa ni pamoja na kuwapa mafunzo wanawake wajasiriamali zaidi ya 300 katika mikoa ya Dar es Salaam, Iringa, Mwanza, Dodoma, Mbeya, Pwani, Kigoma, Kagera na Visiwa vya Zanzibar (Unguja na pemba). 

“Vile vile, washindi 20 miongoni wa wahitimu hao wameweza kupata ruzuku kutoka Serikali ya Marekani - yenye thamani ya Dola 185,000 sawa na shilingi za Tanzania 425,500,000. Fedha hizi zimesaidia kukuza mitaji ya biashara zao. 

“Pia wahitimu wote wameendelea kunufaika na fursa ya msaada wa kitaalamu kutoka kwa wawezeshaji, fursa ya masoko ya biashara zao, kushiriki maonesho ya Sabasaba kwa udhamini wa Ubalozi wa Marekani na kujifunza zaidi nchini Marekani pindi fursa zinapotokea,” ameongeza Dkt Kisyombe. 

Matarajio ya programu hiyo ya AWE, amesema ni kuona washiriki baada ya kuhitimu mafunzo hayo wanakuwa chachu ya maendeleo kwa wanawake wenzao katika maeneo wanakotoka. 

Mafunzo hayo ya miezi mitatu yatafungwa Desemba mwaka huu, kwa mujibu wa Mratibu huyo wa AWE Tanzania. 

#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages