NEWS

Monday 27 May 2024

Wanyamapori zaidi ya 2,000 wanasurika mitego ya nyaya Hifadhi ya Serengeti



Mkuu wa Idara ya Ulinzi wa Hifadhi ya Taifa Serengeti, Afisa Mhifadhi Mkuu Davis Mushi akiwasilisha mada katika warsha hiyo. (Picha na Sauti ya Mara)
----------------------------------------------

Na Mwandishi Maalumu
---------------------------------


Kikosi cha kuzuia mitego ya wanyamapori katika Hifadhi ya Taifa Serengeti, kimeokoa wanyamapori 2,383 waliokuwa wametegwa na majangili kwa nyaya.

Wanyama hao wameokolewa kati ya mwaka 2017 na 2024, kwa mujibu wa Mkuu wa Idara ya Ulinzi wa hifadhi hiyo, Afisa Mhifadhi Mkuu Davis Mushi.

“Wanyama waliokolewa wengi walikuwa ni nyumbu na pundamilia,” Mushi aliliambia gazeti hili mara baada ya kuonesha mafanikio ya kikosi kazi hicho katika warsha maalumu iliyoandaliwa na Shirika la Frankfurt Zoological Society (FZS) mjini Mugumu hivi karibuni.

Kikosi hicho pia kimefanikiwa kukamata nyaya 93,116 zilizokuwa zimetumika kutega wanyamapori mbalimbali katika kipindi hicho hicho.


Kikosi hicho ambacho doria zake zinahusisha wanavijiji chini ya mradi ambao unaolenga kutokomeza ujangili wa mitego hiyo katika hifadhi hiyo ambayo ni kivutio kikubwa cha utalii nchini.

Wanavijii hao hutoka kwenye vikundi vya COCOBA (Community Conservation Banks) wakiwemo ambao wamewahi kujihusisha na vitendo vya uwindaji haramu katika hifadhi hiyo.

“Kikosi kinakuwa na wanakijiji wanne kutoka COCOBA ambao hulipwa na FZS, na wengine walishawahi kufanya ujangili hata kwa miaka mitano,” alifafanua Mushi.

Alisema kikosi hicho kinakuwa na watu wanane wakiwemo askari wa Hifadhi ya Serengeti na wanavijiji ambao hufanya ‘rotation’ ili kufikia vijana wengi zaidi..

Alisema mradi huo ambao pia unahusisha kikosi kingine ambacho kazi yake ni kuzuia mifugo hususan ng’ombe kuingia hifadhi ulianza mwaka 2017 chini ya ufadhili wa FZS.

“Tunawapongeza Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) kwa kushirikisha jamii kuzuia uwindaji haramu na uingizwaji wa mifugo katika hifadhi ya Serengeti,” alisema Meneja Mradi wa FZS- Serengeti, Masegeri Rurai.

FZS ni Shirika la Uhifadhi la Kimataifa lenye makao makuu nchini Ujerumani ambalo limekuwa likisaidia Serikali ya Tanzania kuimarisha masuala ya uhifadhi, huku uhifadhi wa ikolojia ya Serengeti ukiwa moja ya vipaumbele vya shirika hilo kwa takribani miaka 60 sasa.

Warsha iliyoandaliwa na shirika hilo iliwaleta pamoja wadau wa uhifadhi, viongozi wa vijiji na kata vinavyopakana na maeneo ya uhifadhi kutathmini maendeleo ya mradi wake unaolenga kupunguza migogoro ya binadamu na wanyamapori katika wilaya ya Serengeti.
Chanzo: Gazeti la SAUTI YA MARA
#Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages