Na Mwandishi Maalumu
---------------------------------
---------------------------------
Uwepo wa malipo yenye mashaka kwa wazabuni ambao hawakuwa kwenye orodha ya madeni ya Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti kwa mwaka husika, ni moja ya sababu zinazodaiwa kusababisha halmashauri hiyo kupata hati ya ukaguzi yenye mashaka kwa mwaka wa fedha 2022/2023.
Hayo yalibainika katika kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo kilichojadili taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) mjini Mugumu, hivi karibuni.
Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Mkuu wa Mkoa (RC) wa Mara, Kanali Evans Mtambi ambaye alitoa maelekezo kadhaa kwa madiwani na watendaji wa halmashauri hiyo ili kuhakikisha tatizo hilo halijirudii.
"Mmepata hati yenye mashaka baada ya kubainika mapungufu mengi kwenye uandaaji wa hesabu za mwisho, ikiwa ni pamoja na uwepo wa malipo yenye mashaka kwa wazabuni ambao madai yao hayakuwepo kwenye madeni ya halmashauri kwa mwaka husika,” alisema RC Mtambi na kuendelea:
"Hati hiyo imeonesha udhaifu wa mifumo ya udhibiti wa ndani na utendaji kwa ujumla kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, hivyo madiwani mnapaswa kuisimamia kikamilifu menejimenti na kuhakikisha hatua stahiki zinachukuliwa dhidi ya wote wanaosababisha hoja za ukaguzi na ubadhirifu wa mali za umma.”
Aidha, taarifa ya CAG inaonesha kuwa kati ya maelekezo sita yaliyotolewa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa, ni moja lililotekelezwa na kufungwa.
"Niwatake Baraza la Madiwani kusimamia uandaaji wa mpango kazi utakaohakikisha maagizo matano yaliyosalia yanatekelezwa kikamilifu. Kwenye eneo la ununuzi na usimamizi wa mikataba zimebainishwa kasoro mbalimbali zinazohitaji uimarishaji wa mifumo ya udhibiti ya ndani.
“Madiwani mnapaswa kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa miradi ya maendeleo na matumizi ya fedha katika maeneo yenu na pale ambapo mtakapobaini taratibu zinakiukwa msisite kuchkuwa hatua stahiki kwa wahusika kwa wakati.
"Halmashauri inatakiwa kuelekeza fedha za mapato yake ya ndani na zile za wadau wa uhifadhi na utalii kwenye ukamilishaji wa miradi viporo ili wananchi waweze kupata huduma iliyokusudiwa,” alisisitiza RC Mtambi.
UNAWEZA PIA KUSOMA:
- 1.Nyambari Nyangwine awasili India, atangaza bidhaa za Tanzania .
- 2.Mwanahabari kumlipa fidia Waziri Mkuu wa Italia baada ya kufanya mzaha juu ya kimo chake .
- 3.Rais Ruto afanya uteuzi Mawaziri wapya 11 .
- 4. Musoma Vijijini wanavyopiga hatua ujenzi shule za sekondari za kata .
- 5.Rais Samia atembelea Sekondari ya Seminari ya Kaengesa mkoani Rukwa .
- 6. HAIPPA PLC inavyoshagihisha uwekezaji Tanzania .
No comments:
Post a Comment