Meneja Shughuli na Biasahra wa WAMACU Ltd, Olais Piniel (kushoto) na Afisa Kilimo na Usafirishaji wa Ushirika huo, Catherin Gimbika wakifurahia tuzo na cheti walivyotunukiwa katika Maadhimisho ya 13 ya Siku ya Mara yaliyofanyika katika kaunti ya Narok nchini Kenya jana. (Na Mpigapicha Wetu)
Chama Kikuu cha Ushirika cha Wakulima wa Mkoa wa Mara (WAMACU) Ltd, jana kiliibuka mshindi wa pili katika Maadhimisho ya 13 ya Siku ya Mara yaliyofanyika katika kaunti ya Narok nchini Kenya.
Ushirika huo ambao unajihusisha na maendeleo ya mazao ya kahawa na tumbaku katika mkoa wa Mara nchini Tanzania, ulitunukiwa tuzo ya ushindi huo na Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria (LVBC).
Ujumbe wa Tanzania katika maadhimisho hayo yaliyofanyika katika mji wa Sekenani uliongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi.
Siku moja kabla ya kilele cha maadhimisho hayo, wadau mablimbali kutoka mataifa hayo mawili walikutana katika kongamano la kisayansi kuhusu uhifadhi wa ikolojia ya Bonde la Mto Mara lililofanyika katika Chuo Kikuu cha Maasai Mara.
Kaulimbiu ya Maadhimisho hayo kwa mwaka huu inasema “Kwa Pamoja: Tuhifadhi Bonde la Mto Mara kwa Bioanuai Endelevu na Ustahimilivu wa Tabianchi” yaani “Flowing Forward Together: Conserving the Mara Basin Ecosystem for Sustainable Biodiversity and Climate Resilience.”
Nchi za Tanzania na Kenya zimekuwa zikiadhimisha Siku ya Mara Septemba 15 kila mwaka kwa kupokezana, ikiwa ni sehemu ya kuendeleza juhudi za pamoja za uhifadhi endelevu wa Bonde la Mto Mara unaotiririsha maji katika Ziwa Victoria upande wa Tanzania.
No comments:
Post a Comment