NEWS

Monday, 16 September 2024

Tutunze mazingira kuimarisha maendeleo haya ya kijamii, kiuchumi


Mazingira bora yanachangia kuimarisha sekta ya utalii, hasa katika Hifadhi za Taifa ikiwemo Serengeti.

Na Christopher Gamaina
Chris_pressman@yahoo.com

Utunzaji wa mazingira ni suala muhimu linalostahili kupewa kipaumbele kwa maendeleo endelevu ya jamii. Nchini Tanzania, kama ilivyo katika nchi nyingi za Afrika, mazingira yana mchango mkubwa katika maendeleo na maisha ya watu.

Kuimarisha utunzaji wa mazingira kunaweza kuwa na faida kubwa za kijamii na kiuchumi katika taifa lolote duniani.

Makala hii inaangazia kwa kina umuhimu wa utunzaji wa mazingira na jinsi unavyoweza kuboresha maisha ya wananchi na kuchangia katika maendeleo ya kiuchumi nchini Tanzania.

Faida za kijamii
Utunzaji wa mazingira una faida nyingi, ikiwemo ya afya bora kwa jamii. Kwa mujibu wa wataalamu wa afya, mazingira safi yanaweza kupunguza kiwango cha magonjwa yanayosababishwa na uchafuzi wa mazingira. Magonjwa hayo ni pamoja na malaria, kipindupindu na magonjwa ya mfumo wa kupumua.

“Mfano, upandaji wa miti husaidia kupunguza mabadiliko ya hali ya hewa na kuboresha ubora wa hewa, hivyo kupunguza hatari za magonjwa ya kupumua,” anasema Dkt Omchamba Salimba.

Kupungua kwa magonjwa yanayosababishwa na uchafuzi wa mazingira kutapunguza mzigo wa gharama za matibabu kwa jamii, hivyo kuongeza nguvu kazi na kuboresha uchumi wa familia.

Vile vile, kilimo kinachozingatia utunzaji wa mazingira kinaweza kuongeza mavuno na kuimarisha usalama wa chakula, hivyo kuboresha hali ya maisha ya wakulima, kwa mujibu wa wataalamu wa ugani.

Kwa upande mwingine, uhifadhi na matumizi bora ya vyanzo vya maji ikiwemo mito, maziwa na bahari ni muhimu ili kuwezesha upatikanaji wa majisafi na salama kwa ajili ya matumizi ya watu, wanyama na viumbe wengine.

Lakini pia, mazingira bora yanachangia katika uhifadhi wa maeneo ya kihistoria na urithi wa kitamaduni, ambayo ni sehemu muhimu ya utambulisho wa jamii na utamaduni wa nchi.

Faida za kiuchumi
Mazingira bora yanaweza kuimarisha sekta ya utalii, hasa katika Hifadhi za Taifa na Mapori ya Akiba yenye vivutio vingi vya utalii.

Utunzaji wa mazingira unachangia katika kudumisha vivutio vya utalii kama vile wanyamapori, hivyo kuongeza mapato kutoka kwa watalii.

Mazingira yakitunzwa yanaweza kutengeneza fursa za ajira katika maeneo mbalimbali yakiwemo ya uhifadhi wa misitu, kilimo na usimamizi wa rasilimali za maji. Hii inaweza kupunguza changamoto ya ajira na kuongeza kipato cha wananchi.

Sambamba na hilo, utunzaji wa mazingira na kilimo kinachozingatia uhifadhi wa ardhi vinasaidia kuongeza uzalishaji wa mazao, hivyo kupunguza uagizaji wa chakula nje ya nchi na kuongeza mapato ya wakulima.

Mambo ya kuzingatia
Uchafuzi wa mazingita kutokana na shughuli za kibinadamu kama vile ujenzi, uchimbaji madini na kilimo kisichozingatia kanuni za mazingira unaweza kuathiri mazingira.

Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UN Environment) linapendekeza kuwe na uchumi ulio na hewa ya ukaa kwa kiwango cha chini, unaotumia rasilimali kikamilifu na unaojali masilahi ya jamii.

Uelewa mdogo kuhusu umuhimu wa utunzaji wa mazingira unachangia katika uharibifu wa mazingira. Elimu na uhamasishaji ni muhimu ili kuhakikisha kwamba wananchi wanajua faida za kutunza mazingira.

Mikakati ya uhamasishaji wa utunzaji wa mazingira ni pamoja na kuanzisha kampeni za elimu kuhusu umuhimu kutunza mazingira kupitia shule, vyombo vya habari na jamii kwa ujumla.

Mkakati mwingine ni kuimarisha usimamizi wa sheria na kanuni zinazohusiana na utunzaji wa mazingira, ikiwa ni pamoja na adhabu kwa watu wanaokiuka sheria za mazingira.

Bila kusahau umuhimu wa kuanzisha na kuendeleza mipango bora ya usimamizi wa rasilimali za asili, kama vile misitu, maji na ardhi ili kuhakikisha kwamba zinatumika kwa njia endelevu.

Sambamba na kuimarisha ushirikiano na jamii katika kutekeleza miradi ya mazingira na kuhakikisha maamuzi yanayohusiana na mazingira yanashirikisha wananchi wa maeneo husika - kama inavyosisitizwa kwenye Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya Mwaka 2004 (Na.20 ya 2004) sehemu ya 14.

Aidha, kwa mujibu wa Sera ya Taifa ya Mazingira ya Mwaka 2021, Mamlaka za Serikali za Mitaa zinawajibika kujumuisha masuala ya mazingira katika mipango yao ya maendeleo ili kuimarisha ulinzi na uhifadhi wa mazingira.

Hata hivyo, serikali na mashirika yanayojishughulisha na mazingira nchini yamekuwa yakikabiliwa na changamoto ya kifedha katika utekelezaji wa miradi ya utunzaji wa mazingira.

Hii ni changamoto kubwa inayohitaji mipango na mikakati madhubuti na ushirikiano wa kimataifa ili kuhakikisha miradi ya utunzaji wa mazingira nchini inafanikiwa kwa maendeleo endelevu.

Akihutubia Mkutano wa 20 wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati (AMECEA) jijini Dar es Salaam Julai 12, 2022, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan alisisitiza kuwa jitihada zaidi na ushirikiano madhubuti vinahitajika ili kufanikisha utunzaji wa mazingira nchini na Afrika kwa ujumla.

Kwa ujumla, utunzaji wa mazingira ni muhimu kwa maendeleo endelevu ya kijamii, kiuchumi na uboreshaji wa maisha ya watu.

Kwa kuimarisha utunzaji wa mazingira, taifa linaweza kufaidika kwa namna nyingi, ikiwemo kuboresha afya, kuongeza mapato ya utalii na kuimarisha uzalishaji wa mazao ya kilimo.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages