![]() |
Waziri wa Madini, Anthony Mavunde (wa tatu kulia waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa TAMISA, miongoni mwa wengine alipozindua chama hicho jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki. |
Na Mwandishi Wetu,
Dar es Salaam
--------------------------------------
Mazingira rafiki ya uwekezaji yamechochea ukuaji wa sekta ya madini nchini na kutoa fursa kwa Watanzania wanaoshiriki katika mnyororo wa thamani wa sekta hiyo kuchangia kupaisha uchumi wa taifa.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa Chama cha Watoa Huduma na Wasambazaji wa Bidhaa Migodini Tanzania (TAMISA) mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde alisema moja ya fursa kubwa katika sekta hiyo ni manunuzi ya bidhaa na utoaji huduma migodini.
Waziri Mavunde alitumia nafasi hiyo pia kuwahimiza Watanzania wanaoshiriki kwenye manunuzi ya bidhaa na utoaji huduma migodini kuchangamkia fursa hiyo akisema kwa mwaka 2023/2024 shilingi trilioni 3.1 zilitumika katika eneo hilo.
“Natamani sana kuziona hizi trilioni 3.1 zinabaki mikononi mwa Watanzania kuchochea uchumi wa nchi yetu kwa kuanzisha viwanda vya bidhaa na huduma zenye mahitaji makubwa migodini,” alisema.
Alisema TAMISA kitasaidia kuwa na sauti ya pamoja katika kuwajengea uwezo Watanzania na kuwaimarisha ili kuwa washindani katika utoaji wa huduma na usambazaji wa bidhaa migodini.
Aliwapongeza wanachama wa TAMISA kwa kupokea na kuyafanyia kazi maagizo yake ya uanzishwaji wa chama hicho kuwa jukwaa la mafanikio ya sekta binafsi.
Mwenyekiti wa TAMISA, Peter Kumalilwa alisema malengo ya chama hicho ni kuwajengea uwezo Watanzania kunufaika na sekta ya madini kwa kushirikianana serikali.
Naye mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Octavian Mshiu aliipongeza serikali kwa kuvutia wawekezaji katika sekta mbalimbali za uchumi na kuwataka Watanzania kuchangamkia uchumi wa madini.
No comments:
Post a Comment