NEWS

Friday 20 September 2024

Watu 15 mbaroni kwa kuwashambulia askari wa usalama barabarani wakitekeleza majukumu yao wilayani Serengeti




Na Mwandishi Wetu/ Mara Online News

Watu 15 wakiwemo dereva, kondakta, utingo na abiria wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kuwashambulia kwa vipigo askari wawili wa usalama barabarani (trafiki) waliokuwa wakitekeleza majukumu yao wilayani Serengeti.

Watuhumiwa hao wanadaiwa kutenda makosa hayo Septemba 18, 2024 saa 12 jioni katika barabara ya Bunda – Mugumu kijijini Natta, Serengeti wakati trafiki hao waliposimamisha na kuanza kukagua gari lenye namba za usajili T 476 ECP aina ya TATA lililokuwa likitokea jijini Mwanza kwenda Mugumu, Serengeti.

“Baada gari hilo kusimama askari hao waliingia ndani na kuanza kukagua na kubaini lilikuwa limezidisha abiria. Wakati wakiendelea kutekeleza majukumu yao, dereva, kondakta, utingo na baadhi ya abiria walianza kuwashambulia kwa kuwapiga sehemu mbalimbali za miili na kumjeruhi vibaya Koplo Paulo upande wa jicho la kulia.

“Watuhumiwa wote 15 wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa upelelezi zaidi, na mara baada ya upelelezi kukamilika jalada litapelekwa kwa mwendesha mashitaka kwa hatua zaidi,” ilieleza sehemu ya taarifa kwa umma iliyotolewa juzi na Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, ACP Menrad Sindano.

Aidha, jeshi hilo limetoa onyo kali kwa watu wenye tabia ya kujichukulia sheria mkononi - likisisitiza kuwa halitasita kuchukua hatua kali za kisheria dhidi yao.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages