NEWS

Thursday, 19 September 2024

Mtoto wa kike aokolewa katika jaribio ovu Nyamongo, mtuhumiwa atoroka, atelekeza pikipiki




Na Mwandishi Wetu/ Mara Online News
Tarime

Mtoto wa kike anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka sita ameokolewa kutoka mikononi mwa mwanaume aliyekuwa amempora katika kijiji cha Kerende kilichopo Nyamongo wilayani Tarime, Mara kwa sababu ambazo hazijajulikana.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji hicho, Muniko Magabe, tukio hilo limejiri leo Alhamisi mchana na kwamba mtuhumiwa huyo ambaye hajafahamika ametoroka na kutelekeza pikipiki yenye namba za usajili MC 885 CCE.

“Wachimbaji wadogo waliona pikipiki hiyo lakini gafla ikasimama, muda mfupi baadaye wakaanza kusikia mtoto analia kichakani, wakasogea kwenye eneo hilo na kurusha jiwe, ndipo (mtuhumiwa) akatimua mbio na kutelekeza pikipiki na kuacha mtoto,” Magabe ameiambia Mara Online News kwa njia ya simu.

Taarifa zaidi zinaeleza kuwa kabla ya kuondoka na mtoto, mtuhumiwa huyo alionekana akinunua mikate katika moja ya maduka kijijini hapo.

“Lakini tunawashukuru sana wananchi ambao ni wachimbaji wadogo, wakiwemo akina mama kwa kumuokoa huyu mtoto. Sasa hivi ninaenda naye kuripoti kwenye Kituo cha Polisi Nyamongo,” ameongeza kiongozi huyo wa kijiji akiwa anatokea eneo la tukio hilo.

Mara Online News tunaendelea na juhudi za kumpata Kamanda wa Mkoa wa Polisi Tarime Rorya kwa ajili ya kuzungumzia zaidi tukio hilo.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages