NEWS

Friday, 20 September 2024

Taasisi ya Nyambari Nyangwine yazinduliwa kwa kishindo Dar, serikali yaahidi kuiunga mkono, wafanyabiashara maarufu kutoka India washiriki



Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mwanaidi Ally Khamis (katikati waliokaa), Nyambari Nyanwine (mwenye kofia nyekundu) na baafhi ya wageni waalikwa wakifuatilia jambo katika hafla ya uzinduzi wa Taasisi ya Nyambari Nyangwine (NNF) jijini Far es Salaam jana.
----------------------------------------------

Na Mwandishi Wetu/ Mara Online News
Dar es Salaam

Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mwanaidi Ally Khamis amemwakilisha Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa Majaliwa kuzindua Taasisi ya Nyambari Nyangwine (Nyambari Nyangwine Foundation - NNF).

Uzinduzi huo ulifanyika jijini Dar es salaam jana katika hafla iliyofana kwa aina yake na kuhudhuriwa pia na kundi la wafanyabiashara maarufu kutoka nchini India.

Naibu Waziri Mwanaidi akisoma hotuba ya Waziri Mkuu Majaliwa, alimpongeza Mwanzilishi na Mwenyekiti wa NNF, Nyambari Chacha Mariba Nyangwine kwa maono na dhamira yake ya kuleta maendeleo ya kijamii kupitia elimu, ujasiriamali, uhifadhi wa mazingira na kukuza utamaduni wa Mtanzania.

“Nimetiwa moyo kuona mwelekeo thabiti wa taasisi hii [NNF] katika kushughulikia changamoto zinazowakabili vijana na jamii kwa ujumla. Uboreshaji wa elimu ya ujasiriamali, afya, TEHAMA, uhifadhi wa mazingira na ukuzaji wa utamaduni wa Mtanzania, ni mambo muhimu sana kwa ustawi wa taifa letu.

“Juhudi hizi [za Nyambari] zinawiana kikamilifu na mikakati ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. Sisi kama serikali tuna jukumu la kuunga mkono juhudi za taasisi hii na kuwa nao bega kwa bega katika kutimiza maono yao,” alisema Naibu Waziri Mwanaidi. katika hotuba hiyo.

Miongoni mwa malengo ya Taasisi ya Nyambari Nyangwine ni kuunga mkono juhudi za serikali katika uboreshaji wa huduma za elimu na afya, kutengeneza ajira, kukukuza utamaduni wa Mtanzania kikanda na kimataifa huku suala la lugha ya Kiswahili likipewa kipaumbele.

Awali, Nyambari alisema kwa muda mrefu kupitia kampuni zake amekuwa akisaidia umma wa Watanzania katika sekta za elimu, afya, maji na kutoa misaada muhimu ya kibinadamu katika maeneo mbalimbali nchini.

“Hii taasisi ya NNF lengo lake kubwa ni kumsaidia Mtanzania kupiga vita umaskini. Umefika wakati kwa vijana kuchangamkia fursa zinazotolewa na taasisi hii ili wapate ujuzi na maarifa. Kwenye ajira tutasisitiza suala la ujasiriamali kuhusu namna ya kijiajiri,” alisema Nyambari na kuongeza kuwa taasisi hiyo pia itaunga mkono juhudi za serikali katika utangazaji wa vivutio vya utalii vilivyopo nchini.

Siku moja kabla ya unzinduzi huo wa NNF, Nyambari aliongoza kundi la wafanyabishara maarufu kutoka India kumtembelea Rais wa Zanzibar, Dkt Hussein Ali Mwinyi.

Katika mazunguzo yao na Rais Mwinyi, wafanyabiashara hao walionesha nia ya kuwekeza Zanzibar kwenye sekta za utalii ikiwa ni pamoja na ujenzi wa hoteli, hospitali na shule.

“Rais Mhe. Dkt. Mwinyi aliwaahidi ushirikiano mkubwa na mazingira rafiki ya uwekezaji, na kwa upande wa Bara watawekeza kwenye viwanda, shule na utalii,” alisema Nyambari ambaye amewahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Tarime mkoani Mara kupitia chama tawala - CCM.

Nyambari ambaye ni mfanyabishara, mwandishi na mchapishaji wa vitabu maarufu nchini Tanzania, alipokea kundi hilo la wafanyabiashara kutoka India wiki chache baada ya kufanya ziara ya kibiashara ya siku saba nchini India, amanpo alikutana na Waziri wa Utalii wa India, Shri Gajendra Singh Shekhawat na kumpatia zawadi ya bidhaa tofauti kutoka Tanzania kama vile kahawa, korosho, na majarida mbalimbali yanayoonesha vivutio vya utalii vilivyopo kwenye hifadhi za wanyamapori hapa Tanzania.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages