NEWS

Monday 7 October 2024

Butiama ilivyong’ara ziara ya Waziri Simbachawene mkoani Mara



Waziri George Simbachawene (Katikati mbele), Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi (mwenye kofi) na Mbunge wa Butiama, Jumanne Sagini (kushoto kwa Simbachawene) wakiwa na viongozi mbalimbali wa chama na serikali mbele ya jengo la utawala la Shule ya Msingi Chief Manyori kijijini Nyamisisi.
--------------------------------------------

Na Mwandishi Wetu, Butiama

Wiki iliyopita, Waziri wa nchi, Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utwala bora, George Simbachawene alihitimisha ziara yake ya kikazi mkoani Mara, ambapo Halmashauri ya Wilaya ya Butiama ilionekana kung’ara zaidi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya jamii kutokana na fedha za serikali.

Simbachawene alieleza kuridhishwa na miradi iliyokamilishwa na inayoendelea kutekelezwa katika halmashauri hiyo, miongoni mwa halmashauri nyingine mkoani Mara.

Alisema mafanikio hayo yametokana na msukumo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan, ikiwa ni sehemu ya kumuenzi kwa vitendo Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarange Nyerere aliyezaliwa na kuzikwa mkoani humo.

Jengo la utawala la Shule ya Msingi 
Chief Manyori kijijini Nyamisisi.
------------------------------------------

"Hongereni kwa miradi mikubwa ya maendeleo, fedha nyingi zinaletwa hapa kutokana na utashi wa Rais Samia. Mmepata miradi mikubwa ya elimu, afya, chuo kikuu, mradi mkubwa wa maji Mgango-Kiabakari na mradi wa umeme wa Mwalimu Nyerere. Pongezi mlizotoa nitazifikisha kwa Rais," alisema Waziri Simbachawene.

Aliyasema hayo wakati wa ziara yake Butiama ambapo alizindua shule mpya ya msingi ya Chief Manyori iliyojengwa katika kijiji cha Nyamisisi kwa gharama ya shilingi milioni 640 zilizotolewa na serikali.

Awali, akizungumza kwa niaba ya wananchi, Mbunge wa Jimbo la Butiama, Jumanne Sagini alimshukuru Rais Samia kwa kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi iliyokuwa imekwama kwa miaka mitatu, likiwemo jengo la Halmashauri ya Wilaya ya Butiama.

"Tunaipongeza serikali kwa ilichowafanyia wananchi wa Nyamisisi kwa kujenga shule mpya ili kuwezesha kila mtoto kupata elimu.

"Jengo la Halmashauri limekuja kukamilishwa na Dkt Samia, lakini pia serikali imetujengea sekondari mpya nane, shule za msingi 12, kituo cha afya Kiagata, pamoja na ujenzi wa Chuo Kikuu cha Kilimo na Teknolojia," alisema Sagini ambaye pia ni Naibu Waziri wa Katiba na Sheria.

Waziri George Simbachawene akifurahia kucheza ngoma ya asili pamoja na kikundi cha wasanii kilichoandaliwa kutumbuiza wakati wa ziara yake wilayani Butiama. (Picha zote na Mara Online News)
-----------------------------------------

Naye Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi alimshukuru Rais Samia kwa kupeleka fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya wananchi.

"Haijawahi kutokea mkoa wa Mara umepata trilioni moja na bilioni 220 kwa ajili ya miradi 280 inayoendelea kutekelezwa, haitakaa itokee kupata Rais kama Samia, kila sehemu amegusa," alisema Mtambi.

Katika ziara hiyo pia Waziri Simbachawene alizungumza na wananchi katika mikutano ya hadhara ambapo pamoja na mambo mengine aliwahimiza kujitokeza kwa wingi kujiandikisha kwa ajili ya kushiriki uchaguzi wa viongozi serikali za mitaa.

Mkoa wa Mara unatajwa kupata mafanikio makubwa katika utekelezaji wa miradi mingi ya maendeleo katika sekta za afya, elimu, maji na miundombinu ya barabara.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mara, Patrick Chandi Marwa, miradi inayotekelezwa ni kielelezo cha kutimiza azma ya serikali ya kusogeza na kuboresha huduma za afya kwa wananchi, ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya chama hicho tawala ya mwaka 2020-2025.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages