NEWS

Sunday 6 October 2024

Rais wa Barrick akabidhi shule mpya ya kisasa iliyojengwa na mgodi wa North Mara



Rais na CEO wa Barrick, Dkt Mark Bristow (mwenye kofia) akiwasili kukabidhi Shule ya Msingi mpya Kenyangi iliyojengwa na Mgodi wa Dhahabu wa North Mara, katika hafla iliyofanyika shuleni hapo leo Oktoba 6, 2024. (Picha na Mara Online News)
---------------------------------------------

Na Mwandishi Maalumu/ Mara Online News

Rais na Afisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa Kampuni ya Barrick, Dkt Mark Bristow amekabidhi kwa uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime shule ya msingi mpya ya kisasa iliyojengwa na Mgodi wa Dhahabu wa North Mara.

Shule hiyo imejengwa katika kijiji cha Matongo, jirani na mgodi huo unaoendeshwa na Kampuni ya Barrick kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia Kampuni ya Twiga Minerals.

Mgodi wa North Mara umejenga shule hiyo ili kuhamisha Shule ya Msingi Kenyangi kwa ajili ya kupisha upanuzi wa shughuli zake.

“Ninaishukuru jamii ya hapa kwa ushirikiano mkubwa uliotuwezesha kufanikisha utekelezaji wa mradi huu, na ninawatakia kila la heri wanafunzi wanaokuja kusoma hapa,” amesema Dkt Mark katika hafla ya kukabidhi shule hiyo leo Oktoba 6, 2024.

Rais na CEO huyo wa Barrick amesisitiza umuhimu wa uwekezaji kwenye sekta ya elimu kwa maendeleo ya jamii inayozunguka mgodi huo na bara la Afrika kwa ujumla. “Kusherekea uwekezaji wa shule hii ni kusherekea Afrika ya baadaye,“ amesema.

Rais na CEO wa Barrick, Dkt Mark Bristow akiwa katika picha ya pamoja na viongozi mbalimbali na wanafunzi baada ya kukabidhi Shule ya Msingi mpya Kenyangi.
----------------------------------------------

Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini, Mwita Waitara amemshukuru Dkt Mark na kumueleza kuwa shule hiyo ni miongoni mwa miradi mikubwa ya kijamii iliyojengwa kutokana na fedha za mgodi wa North Mara.

“Dkt Mark tunakusukuru sana kwa shule hii, na hii ni miongoni mwa shule bora katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, watoto watasoma katika mazingira mazuri,” amesema Waitara.

Naye Diwani wa Kata ya Matongo, Godfrey Kegoye ameshukuru akisema ubora wa shule hiyo utachochea ukuaji wa taaluma kwa wanafunzi.

“Tunamshukuru sana Dkt Mark kwa sababu vitu vyote anavyoahidi anavitekeleza kwa vitendo, tunamwombea baraka kwa Mungu,” amesema Kegoye.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kenyangi, Hadija Nusura naye ameshukuru akisema “Mgodi umetujengea shule nzuri sana, kwa kweli tunapaswa kujivunia mgodi huu.”

Awali, Dkt Mark amepata fursa ya kujionea miundombinu ya shule hiyo na kupanda mti wa asili kama ishara ya Mgodi wa North Mara kuunga juhudi za uhifadhi wa mazingira.

Hafla ya kukabidhi shule hiyo imehudhuriwa pia na Meneja wa Barrick nchini Tanzania, Dkt Melkiory Ngido, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Paragia Balozi, Meneja Mkuu wa Mgodi wa North Mara, Apolinary Lyambiko, Meneja Mahusiano wa mgodi huo, Francis Uhadi, madiwani, wenyeviti wa vijiji, wazee wa mila na wanafunzi.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages