Na Mwandishi Wetu
Jeshi la Polisi Mkoa wa Tarime Rorya kwa ushirikiano na wadau wake mbalimbali liamezindua kampeni ya Tuwambie Kabla Hawajaharibiwa inayowalenga vijana/ wanafunzi, hususan wanaotarajia kuanza kidato cha kwanza na cha tano.
Kampeni hiyo ilizinduliwa jana Oktoba 4, 2024 ambapo ilianza kwa maandamano katika maeneo ya mji wa Nyamongo iliongozwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tarime Rorya, SACP Mark Njera akiambatana na Mkuu wa Polisi Jamii wa mkoa huo, ACP Jumanne Mkwama.
Aidha, kampeni hiyo ilishirikisha wadau mbalimbali ambao ni pamoja na Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara, Jeshi la Magereza, Idara ya Uhamiaji, WiLDAF, ATFGM-Masanga, Kivulini, viongozi wa Serikali, madhehebu ya dini, walimu na wanafunzi wa shule za msingi na sekondari.
Katika hotuba yake, Kamanda Njera alisema "Kampeni hii inalenga kuwasaidia vijana kujiamini, kuishi ujana kwa kujali utu wao na utu wa wengine, kujitunza, kuzingatia maadili mema, kutambua namna ya kukabiliana na ukatili na kutatua changamoto za ujana, kuwa wazalendo kwa nchi yao na kuheshimu mila na desturi nzuri za jamii," Kamanda Njera alisema katika hotuba yake.
Kamanda Njera aliongeza kuwa kampeni ya Tuwambie Kabla Hawajaharibiwa imeanzishwa na Jeshi la Polisi kwa lengo lingine la kuwatahadharisha wanafunzi na wanachuo wanaojiunga na masomo kuacha kuiga tabia mbaya kutoka kwa wenzao waliowatangulia, kwani zinaweza kuzima ndoto zao za kielimu na kuwaharibia mustakabali wa maisha yao ya baadaye.
Aidha, Kamanda huyo aliwashukuru wadau wote kwa kuunga mkono kampeni hiyo yenye tija kwa vijana wa Kitanzania.
UNAWEZA PIA KUSOMA:
>>Rais wa Barrick akabidhi shule mpya ya kisasa iliyojengwa na mgodi wa North Mara
>>Naibu Rais Rigathi Gachagua aomba msamaha kwa Rais Ruto
>>Waziri Simbachawene azindua shule mpya iliyogharimu milioni 640/- Butiama, Sagini amshukuru Rais Samia
>>Katibu CCM Mara afungua kambi la mafunzo kwa vijana wa UVCCM, awataka kutokubali kutumiwa kuvuruga amani
No comments:
Post a Comment