NEWS

Tuesday 8 October 2024

Mary Daniel afunga mafunzo ya vijana wa UVCCM Mara, ahimiza uzalendo kwa taifa





Viongozi wa UVCCM Mkoa wa Mara wakiongozwa na Mwenyekiti wao, Mary Daniel Joseph (katikati asiye na kofia) wakati wa ufungaji wa kambi la mafunzo kwa Vijana wa umoja huo wilayani Butiama leo Oktoba 8, 2024. (Picha na Mara Online News)
 --------------------------------------------

Na Godfrey Marwa/ Mara Online News,
Butiama

Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoa wa Mara, Mary Daniel Joseph amefunga kambi la mafunzo kwa vijana zaidi ya 1,400 wa umoja huo na kusisitiza uzalendo kwa taifa.

Aidha, amesema umoja, upendo na mshikamano baina ya vijana hao ni muhimu, hasa kipindi hiki cha kuelekea kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa baadaye mwaka huu na Uchaguzi Mkuu mwakani ili kukiwezesha chama hicho tawala kupata ushindi wa kishindo.

Mary ameyasema hayo katika hotuba yake ya kufunga kambi la mafunzo hayo ya siku saba katika Chuo cha VETA Wilaya ya Butiama, mkoani Mara leo Oktoba 8, 2024.

"Muwe na uzalendo na morali huu mtakapoanza matembezi kwenda Mwanza. Ninawaona mnavyojitoa ni uzalendo wa hali ya juu," amesema na kuendeleza:

"Hata baada ya kuhitimisha matembezi katika kilele cha mbio za Mwenge tuendelee kushikamana, rafiki uliyempata leo usimfanye kuwa adui wala kumpoteza.

"Umoja wetu ni popote tunapokuwa, itatusaidia safari tunayoenda maana lengo la CCM ni kushika dola."

Mwenyekiti huyo wa UVCCM Mkoa wa Mara ametumia nafasi hiyo pia kuwakumbusha vijana hao kuwa siasa ya CCM ni pamoja na uchumi, hivyo wanapaswa kuchangamkia asilimia 10 ya fedha za mapato ya ndani inayotengwa na kila halmashauri kwa ajili ya mikopo kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu.

"Mara kuna bilioni mbili kwa ajili ya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu,," amedokeza Mary.

Naye Katibu Idara ya uhamasishaji na Mafunzo CCM Taifa, Kashmir Haji Makame amewataka vijana hao kuzingatia suala la nidhamu kwa manufaa yao na taifa. "Hakuna kitu kizuri kama nidhamu. Heshimu kila mtu hata asiyekuwa kiongozi wako,," amesema Makame.

Kambi hilo limefungwa tayari kwa vijana hao kutoka mkoa wa Mara kuanza matembezi ya kilometa 284 kwenda mkoani Mwanza kushiriki kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, sambamba na miaka 25 ya kumbukumbu ya kifo cha Baba wa Taifa la Tanzania Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages