NEWS

Tuesday, 19 November 2024

Rais Samia aongeza saa 24 za kuwaokoa wahanga wa jengo la Kariakoo





Na Mwandishi Wetu
----------------------------

Rais Samia Suluhu Hassan amemwelekeza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, kuongeza saa 24 zaidi za kuendelea kuwatafuta watu waliofukiwa na kifusi kwenye jengo la ghorofa lililoporomoka Jumamosi iliyopita eneo la Kariakoo jijini Dar es Salaam.

Rais ametoa agizo hilo leo wakati akizungumza na Waziri Mkuu kwa njia ya simu kutoka Rio de Janeiro, Brazil, anakohudhuria mkutano wa mataifa tajiri duniani -- G 20.

"Nimemwelekeza (Waziri Mkuu) kuwa ninatambua uokoaji katika majanga una muda maalum wa saa 72 mpaka unapositishwa. Licha ya utaratibu huo, binafsi nina matumaini kuwa Mwenyezi Mungu huweka mkono wake kwenye changamoto za aina hii, hivyo basi nimemwelekeza kuongeza saa 24 kwenye zoezi hili ili kuendelea kuwapambania ndugu zetu ambao tunaamini bado wako hai. Baada ya saa 24 hizo kumalizika tufanye tathmini ya kina kabla ya maamuzi yoyote juu ya mwelekeo wa zoezi hilo," alisema Rais katika mazungumzo na Waziri Mkuu.

Aliongeza: "Maisha na uhai wa kila binadamu ni zawadi ya kipekee toka kwa Mwenyezi Mungu na kama taifa uhai na maisha ya Mtanzania yeyote ni lazima kupiganiwa kwa nguvu zote."

Rais amewataka Watanzania wote mahali walipo waendelee kuwaombea wahanga waliokwama kwenye kifusi cha jengo lililoporomoka na pia kuviombea vikosi vinavyoendelea na kazi ya uokoaji kwenye eneo la tukio.

Watu zaidi ya 10 wamekufa na wengine zaidi ya 90 walijeruhiwa katika tukio hilo, takwimu ambazo zimekuwa zikibadilika kila wakati jinsi zoezi la uokozi linavyoendelea.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages