NEWS

Wednesday, 20 November 2024

Barrick yatunukiwa tuzo ya kudhamini mkutano wa kimataifa wa madini



Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa (katikati) akikabidhi cheti cha tuzo ya udhamini mkuu wa mkutano wa kimataifa wa sekta ya madini kwa Meneja wa Barrick nchini, Melkiory Ngido jijini Dar es Salaam jana. Kushoto ni Waziri wa Madini, Anthony Mavunde.
---------------------------------------------

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

KAMPUNI ya Barrick jana ilitunukiwa tuzo ya kuwa mdhamini mkuu wa mkutano wa kimataifa wa madini unaofanyika jijini Dar es Salaam.

Tuzo hizo kwa kampuni zilizodhamini mkutano huo mkubwa zilikabidhiwa kwa wawakilishi wa kampuni husika na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ambaye alikuwa mgeni rasmi akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais Dkt Samia Suluhu Hassan.

Kampuni ya Barrick, inayoendesha migodi ya dhahabu nchini kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia Kampuni ya Twiga Minerals, imekuwa mstari wa mbele katika kuchangia maendeleo ya kijamii.

Akizungumza katika mkutano huo kabla ya kukabidhiwa tuzo hizo, Meneja wa Barrick nchini Tanzania, Melkiory Ngido aliwaeleza wajumbe wa mkutano huo jinsi ubia wa Barrick na Twiga unavyoendelea kupata mafanikio makubwa na kuwa mfano wa kimataifa unaodhihirisha kuwa Serikali inaweza kushirikiana na sekta binafsi na kuleta mapinduzi makubwa ya kiuchumi.

Ngido alisema kwamba katika kipindi kifupi ubia huo umeweza kuchangia pato la taifa kwa kiasi kikubwa kupitia kodi na tozo mbalimbali za Serikali na kuongeza ajira kwa Watanzania.

Pia, kufanikisha miradi mikubwa ya kijamii, hususan katika sekta za barabara, afya, maji na elimu pamoja na kufanikisha kuinua uchumi wa wazabuni wa Kitanzania wanaouza bidhaa mbalimbali kwenye migodi yake ya North Mara, Bulyanhulu na Buzwagi.

Wakati huo huo, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde aliuambia mkutano huo kwamba kati ya mwaka 2021 na mwaka 2024 sekta ya madini imechangia pato la taifa kwa asilimia 7.2 hadi asilimia 9.0.

Mavunde alisema katika mwaka wa fedha 2024/2025, kwa siku 135 sekta hiyo imeingiza shilingi bilioni 392 katika Mfuko Mkuu wa Serikali.

Lengo la Serikali ifikapo Juni 2024 ni sekta hiyo kuingiza shilingi trilioni moja, Mavunde aliufahamisha mkutano.

Waziri huyo alisema kutokana na ongezeko la bajeti ya Wizara ya Madini kutoka shilingi bilioni 89 hadi bilioni 231, kiwango kikubwa cha bajeti hiyo kimeelekezwa kwenye taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini kwa ujenzi wa maabara ya kisasa mkoani Dodoma na mikoa ya kimadini ya Geita na Chunya.

Hali kadhalika, Mavunde alisema Serikali imetenga fedha kwa ajili ya ununuzi wa helikopta itakayosaidia utafiti wa kina.

Mpaka sasa Serikali imefanya utafiti wa kina kwa asilimia 16, ambapo Tanzania ina eneo la kilomita za mraba 945,000, sawa na ekari milioni 233.

"Tumejiwekea malengo ifikapo mwaka 2030 tuwe tumefika eneo lenye ukubwa wa asilimia 50 ya nchi yetu," alifafanua Waziri huyo.

Mavunde alisema katika asilimia 16 iliyofanyiwa utafiti kwa mwaka 2022/2023, sekta ya madini iliongoza kwa kuingiza Dola za Marekani bilioni 3.1, sawa na asilimia 56 ya fedha za kigeni zilizopatikana nchini.

Lengo la mkutano wa madini na uwekezaji ni kuichochea sekta ya madini nchini kuongeza mchango wake katika ukuaji wa uchumi kwa kuhakikisha inachangia asilimia 10 ya pato ka taifa.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages