NEWS

Tuesday, 19 November 2024

Kamati ya Rufani Tarime yarejesha wagombea 100, CHADEMA, ACT Wazalendo waipongeza



Mwenyekiti wa Kamati ya Rufani ambaye pia ni Katibu Tawala wa Wilaya ya Tarime, Mwalimu Saul Mwaisenye akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) ofisini kwake leo Novemba 19, 2024. (Picha na Mara Online News)
-------------------------------------------

Na Christopher Gamaina
Mara Online News

Kamati ya Rufani Wilaya ya Tarime, mkoani Mara imewarejesha wagombea 100 kutoka CHADEMA, ACT Wazalendo na CCM waliokuwa wamewekewa pingamizi kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

Kamati hiyo imetupilia mbali pingamizi zilizowasilishwa dhidi ya wagombea hao baada ya kuzipitia na kubaini hazikuwa na msingi wa kikanuni, au zilikuwa na changamoto ndogo ndogo ambazo haziwaondolei sifa za kugombea uongozi.

“Kwa wilaya nzima ya Tarime tulipokea rufani 128 za wagombea kutoka CHADEMA waliokuwa wameenguliwa na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi, kati ya hao, tuliwarejesha 90, na rufani 36 tulizitupilia mbali.

“Pia, tulipokea rufani tisa kutoka CCM ambapo tatu zilikubaliwa, sita tulizikataa. Kwa upande wa ACT Wazalendo tulipokea rufani saba na zote tulizikubali na kuagiza wagombea husika warejeshwe kwenye mchakato ili wakapambane kwenye boksi la kura,” Mwenyekiti wa Kamati ya Rufani Wilaya ya Tarime, Mwalimu Saul Mwaisenye amewambia waandishi wa habari ofisini kwake leo Novemba 19, 2024.

Mwaisenye ambaye pia ni Katibu Tawala wa Wilaya (DAS) ya Tarime, amesema Kamati ya Rufani iliamua kuwarudisha wagombea hao baada ya kubaini walikuwa na dasari ndogo ndogo kama vile kutoandika majina ya vijiji, au vitongoji wanavyogombea.

“Wengine herufi za majina zilipishana kama vile kuchanganya R na L. Lakini wapo waliodaiwa kuchelewa kurudisha fomu za kugombea, hawa baada ya kufuatilia ilionekana famu zao zilipokewa, hivyo kwa kuwa zilipokewa tuliamini waliziwasilisha ndani ya muda mwafaka,” ameongeza.

Kuhusu rufani 36 za CHADEMA na sita za CCM zilizotupiliwa mbali, Mwaisenye amesema zilikuwa za wagombea ambao hawakukidhi matakwa ya kikanuni.

“Sababu zilizofanya tusizikubali rufani hizo ni pamoja na wagombea husika kutojiandikisha kwa ajili ya kupiga kura. Usipojiandikisha unakuwa umepoteza sifa za kushiriki kwenye huu uchaguzi, yaani kupiga kura na kugombea uongozi,” amesema.

Ameongeza “Lakini pia walikuwepo wagombea ambao walikuwa na maslahi na kijiji. Kanuni zetu zinamka mtu anayegombea asiwe na maslahi yoyote na kijiji.”

Mwenyekiti huyo wa Kamati ya Rufani amesema wagombea wengine ambao rufani zao ziligonga mwamba ni ambao uraia una mashaka na waliowahi kufungwa kifungo kinachozidi miezi sita.

“Kwa hiyo, nitoe rai kwa vyama vya siasa ambavyo vimekamilisha taratibu, wagombea wao washiriki kwenye kampeni katika hali ya usalama. Sisi Kamati ya Rufani tulishamaliza kazi yetu, na tulijitahidi kusimamia haki. Mfano kati ya wagombea 128 kutoka CHADEMA waliokuwa wameenguliwa, kurudisha 90 sio jambo dogo,” amesema.

Kwa upande wao baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa ambavyo wagombea wao wameshinda rufani, wameipongeza Kamati ya Rufani Wilaya ya Tarime wakisema imeonesha umakini katika kushughukia suala hilo.

“Ukweli ni kwamba tumetendewa haki kwa hao wagombea waliorejeshwa kwa sababu wametimiza sifa zote za kugombea, sababu za kuondolewa hazikuwa na mashiko yoyote,” amesema Mwenyekiti wa CHADEMA Kanda ya Serengeti inayoundwa na mikoa ya Mara, Simiyu na Shinyanga, Lucas Ngoto ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA Taifa.

Naye Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Mkoa wa Mara, Charles Mwera amesema “Ni kweli tulikata rufaa, majina ya wagombea tuliyopeleka tumeshinda. Kwa kweli tunashukuru kwamba Kamati ya Rufani imefanya kazi vizuri, DAS ameonesha ushirikiano mkubwa.”

Viongozi hao wamesema uamuzi uliotolewa na kamati hiyo utakuwa na manufaa makubwa kwa demokrasia katika uchaguzi ujao wa Serikali za Mitaa wilayani Tarime.

Aidha, wameutazama uamuzi huo kama ishara ya ushindi katika vita vya kisiasa, na wanatarajia kuwa uchaguzi utakuwa na ushindani wa kweli, ambapo wagombea watakuwa huru kuuza sera zao kwa wapiga kura.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages