NEWS

Monday, 20 January 2025

Maamuzi: Mkutano Mkuu CCM wawateua Samia, Mwinyi kugombea urais 2025



Rais Dkt Samia Suluhu Hassan 
na Rais Dkt Hussein Ali Mwinyi.
----------------------------------------

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Mkutano Mkuu Maalum wa CCM Taifa, umepitisha azimio la kumteua Mwenyekiti wa chama hicho tawala, Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea wa nafasi ya urais katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 2025.

Mkutano huo pia ulimpitisha Rais wa Zanzibar, Dkt Hussein Ali Mwinyi kugombea urais katika uchaguzi mkuu uhao.

Mkutano Mkuu wa CCM Taifa ndicho chombo cha mwisho cha maamuzi ya uteuzi wa mgombea wa urais kupitia chama hicho.

Awali, mkutano huo ambao ulifanyika jana Januari 19, 2025 jijini Dodoma, ukiongozwa na Rais Samia, ulipokea na kujadili taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2020-2025 kwa upande wa Zanzibar na Tanzania Bara.

Rais mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete, akizungumza kama mmoja wa wazee wa CCM katika mkutano huo, alisema CCM kina mamlaka ya kujichagulia mgombea wao wakati wowote.

Uamuzi huu wa kihistoria unaonesha imani na matumaini makubwa ambayo wana-CCM wanayo kwa uongozi thabiti na wa kimkakati wa Rais Samia na Rais Mwinyi, pamoja na dhamira yao isiyotetereka ya kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya chama hicho.

Nchimbi mgombea mwenza
Wakati huo huo, Rais Samia amemteua Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Dkt Emmanuel John Nchimbi kuwa mgombea mwenza wake katika Uchaguzi Mkuu ujao.

Rais Samia na Katibu Mkuu 
Nchimbi wakipongezana.
----------------------------------------

Kwa mujibu wa Rais Samia, Makamu wa Rais wa sasa, Dkt Philip Isdor Mpango alimuomba apumzike na ameridhia, ndio maana amemteua Nchimbi.

Hata hivyo, Dkt Mpango ataendelea na majukumu yake kama Makamu wa Rais mpaka Uchaguzi Mkuu utakapofanyika. Hali kadhalika, na Dkt Nchimbi ataendelea na majukumu yake ya Katibu Mkuu wa CCM hadi wakati huo.

Marais wote wawili; Dkt Samia na Dkt Mwinyi wanamaliza awamu zao za kwanza za uongozi mwaka huu. Na kwa mujibu wa utamaduni wa chama hicho, marais walio madarakani huwa hawapatiwi ushindani katika kupewa tiketi ya kugombea urais kwa awamu ya pili.

Rais Samia aliingia madarakani Machi 2021 mara baada ya kifo cha aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Pombe Magufuli. Aliingia madarakani kwa mujibu wa katiba akiwa ndiye mrithi wa urais, kwa nafasi aliyokuwa nayo kipindi hicho ya Makamu wa Rais.

Katika kipindi chake cha uongozi, Tanzania imeshuhudia mafanikio makubwa katika ukuaji wa uchumi, ujenzi wa miundombinu, maboresho ya huduma za afya, na kukuza demokrasia kupitia falsafa yake ya R nne (4R) ya Rais Samia inayojikita katika masuala ya Maridhiano (Reconciliation), Ustahamilivu (Resilience), Mageuzi (Reforms) na Kujenga upya Taifa (Rebuilding).

Akiwa Rais wa kwanza mwanamke katika historia ya Tanzania, Rais Samia si tu kwamba amevunja vikwazo vya kijinsia, bali pia ameweka viwango vipya vya uongozi shirikishi na wa maono.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages